Solskjaer atuliza mashabiki wenye hasira

MANCHESTER, ENGLAND. MASHABIKI wa Manchester United, leo, Alhamisi asubuhi wameingia kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo ikiwa ni moja ya harakati za kupinga michuano ya  European Super League.
Kiasi cha mashabiki 20 walioonekana kuwa na hasira walifanikiwa kuingia kwenye uwanja wa  Aon Training Complex uliopo Carrington ikiwa ni masaa machache kabla ya mazoezi ya kikosi cha kwanza cha wachezaji wa timu hiyo kuanza.
Mashabiki hao waliwapita walinzi na wakatembea hadi mbele ya mlango wa kiwanja cha mazoezi wakiwa na mabango kadhaa na moja wapo ni lile lililoandikwa 'Glazers out' wakiwa na maana ya kuhitaji familia inayomiliki hisa nyingi za timu hiyo kuachia madaraka.
Bango la pili lilisomeka “51 % MUFC 20” likiwa na maana ya kuhitaji utumike mfumo unaotumiwa na timu za Ujerumani ambapo mashabiki ndio huwa na hisa nyingi  kuliko mmiliki.
Taarifa zinadai baada ya mashabiki hao kusimama kwenye mlango wa kuingilia ilimlazimu  Ole Gunnar Solskjaer kuzungumza nao na baada ya muda walimuelewa na wakapisha wachezaji waingie ndani  kwa ajili ya kuendelea na mazoezi.
Kikundi hicho cha mashabiki kimeonyesha hisia zao hizo ikiwa ni masaa  24 baada ya makamo Mtandaji mkuu wa timu hiyo, Ed Woodward kutangaza kwamba ataondoka mwisho wa msimu huu.