Sneijder achambua kinachomtesa Wirtz
Muktasari:
- Wirtz, aliyesajiliwa kwa Pauni 116 milioni akitokea Bayer Leverkusen kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi ameonyesha hana jipya kabisa ndani ya uwanja tangu asajiliwe.
LONDON, ENGLAND: STAA wa zamani wa Real Madrid na Galatasaray, Wesley Sneijder amefunguka kumzungumzia kiungo ghali wa Liverpool, Florian Wirtz, ambaye amesema amekuwa kwenye wakati mgumu kuzoea mazingira ya Ligi Kuu England.
Wirtz, aliyesajiliwa kwa Pauni 116 milioni akitokea Bayer Leverkusen kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi ameonyesha hana jipya kabisa ndani ya uwanja tangu asajiliwe.
Kiungo huyo Mjerumani alikuwa kwenye kiwango bora sana alipokuwa akikipiga Bundesliga na alionekana angeenda kuwa gumzo huko kwenye Ligi Kuu England, lakini badala yake mambo yamekuwa tofauti kabisa.
Kiungo huyo bado hajafunga wala kuasisti katika mechi 11 alizochezea Liverpool kwenye Ligi Kuu England, takwimu ambazo zimeibua gumzo kwenye timu hiyo.
Akzungumzia suala hilo, Sneijder amesema hadithi ya Wirtz ni kitu cha kawaida hasa linapokuja suala la ubora kwenye Ligi Kuu England.
“Siku zote nimekuwa nikisema kuhusu wachezaji wa kutoka Ujerumani na Uholanzi. Akili zao zinafanana. Unaweza kucheza soka zuri kwenye nchi yako, lakini unaweza kuwa na tatizo la kwenda kuzoea kwenye nchi nyingine. Wachezaji wa Kidachi na Kijerumani wapo hivyo, na hilo ndilo ninaloliona linalomtokea Florian Wirtz kwa sasa,” amesema.
“Alionekana kuwa kwenye utulivu mkubwa Ujerumani. Alikuwa mahali mwafaka. Sasa amepiga hatua kubwa zaidi, lakini kwenye klabu kubwa huhitaji muda mwingi kuzoea. Unapaswa kufanya vizuri kwa wakati huohuo.
“Kama unataka kwenda klabu kubwa ukiwa staa mkubwa unapaswa kuanza kuonyesha viwango kwa haraka sana baada ya kusajili, kama huonyeshi, watu hawajali wewe ni nani.”
Liverpool kwa sasa imeachwa pointi nane na vinara Arsenal kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England na imepitwa hadi na mahasimu wao Manchester United kwa tofauti ya mabao ya kufunga kwenye msimamo wa ligi hiyo.