Fjortoft amkingia kifua Wirtz, awashangaa wanaomlaumu
Muktasari:
- Liverpool ilimsajili Wirtz kutoka Bayer Leverkusen majira ya kiangazi kwa ada ya pauni 116 milioni, huku wengi wakitarajia angeweza kuendeleza kiwango chake kama ilivyokuwa kwenye ligi ya Ujerumani.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Norway, Jan Aage Fjortoft, amemtetea kiungo wa Liverpool, Florian Wirtz, akisema mchezaji huyo wa Kijerumani analaumiwa kwa kila jambo linalokwenda vibaya ndani ya klabu, lakini yeye hana wasiwasi wowote kuhusu kiwango chake.
Liverpool ilimsajili Wirtz kutoka Bayer Leverkusen majira ya kiangazi kwa ada ya pauni 116 milioni, huku wengi wakitarajia angeweza kuendeleza kiwango chake kama ilivyokuwa kwenye ligi ya Ujerumani.
Hadi sasa, kiungo huyo ametoa asisti moja tu katika mechi 10 alizocheza kwenye mashindano yote msimu huu, na hakuna hata moja katika Ligi Kuu ya England, hali ambayo imepelekea kulaumiwa na mashabiki wengi wa Liverpool.
Zaidi ya hapo, kikosi cha Arne Slot kimepoteza mechi zake tatu za mwisho mfululizo katika mashindano yote, hali iliyoongeza shinikizo na uchunguzi wa karibu kutoka kwa mashabiki na wachambuzi.
Jan Aage Fjortoft, ambaye aliwahi kucheza Bundesliga akiwa na Eintracht Frankfurt, amezungumza kupitia The Mirror, akisema kuwa hana hofu kabisa kuhusu Wirtz.
“Lawama zote zimeelekezwa kwa Wirtz, inaonekana kana kwamba yeye ndiye anayehusika na kila kitu kibaya ndani ya Liverpool. Kitu pekee kinatakiwa kwa sasa ni kuilaumu timu yote ambayo haifanyi vizuri, lakini sio kwa mchezaji mmoja.
“Kati ya usajili wote wa Ligi Kuu kama Gyökeres, Isak na wengine, mimi nina wasiwasi mdogo kabisa kuhusu Wirtz. Kusajiliwa kwake ni mradi wa muda mrefu, yaani ninaitazama miaka mitano au zaidi,” amesema.
Wirtz ametoa asisti moja pekee msimu huu katika kipigo cha mikwaju ya penalti dhidi ya Crystal Palace kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, baada ya hapo hajatoa mchango wowote wa bao katika mechi tisa mfululizo.
Jan Aage Fjortoft amesisitiza kuwa Wirtz bado ni mchezaji wa muda mrefu na anatakiwa kuaminiwa, licha ya changamoto za awali katika maisha yake ya soka ndani ya Anfield.