Slot amfikiria Ekitike gemu la Arsenal
Muktasari:
- Ekitike aliachwa nje ya kikosi cha Liverpool kilichocheza dhidi ya Fulham kwenye Ligi Kuu England, Jumapili kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot ana matumaini kuwa straika Hugo Ekitike atakuwa fiti kiasi cha kutosha kuwakabili Arsenal baada ya kukosa uhakika kama staa huyo atarejea kwa wakati.
Ekitike aliachwa nje ya kikosi cha Liverpool kilichocheza dhidi ya Fulham kwenye Ligi Kuu England, Jumapili kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja.
Slot alithibitisha kuwa tatizo hilo lilitokana na idadi kubwa ya dakika alizolazimika kucheza Ekitike kutokana na kutokuwapo kwa straika Alexander Isak.
Isak alikumbwa na tatizo la kuvunjika mfupa mdogo wa mguu wakati wa mchezo dhidi ya Tottenham Hotspur kabla ya Krismasi, jambo lililomfanya Ekitike kuwa chaguo pekee la kocha Slot katika nafasi ya ushambuliaji.
Baada ya kukosa kikosi kilichosafiri kwenda Craven Cottage, kuna wasiwasi juu ya uwezekano wa Ekitike kutumika kwenye mechi dhidi ya vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal, Alhamisi hii.
Hata hivyo, jambo linalotia wasiwasi zaidi ni uwezo wa Ekitike kudhibiti mzigo wa kazi anapozidi kuzoea maisha ya Ligi Kuu England, hasa ikizingatiwa kuwa Isak hatarajiwi kurejea hivi karibuni.
“Alexander Isak amekuwa nje kwa wiki kadhaa sasa, na hilo limemaanisha Hugo amelazimika kucheza dakika nyingi zaidi kuliko alivyocheza katika msimu mzima,” amesema Slot.
“Hilo limesababisha apate jeraha dogo la misuli ya paja kwa sababu tulilazimika kumtumia mara kwa mara kwa dakika nyingi.
“Kwa mchezaji wa umri wake ambaye bado hajaizoea kikamilifu Ligi Kuu, hilo limekuwa mzigo mkubwa kidogo. Ndiyo maana hayupo leo, na tunatumaini atarejea kwenye mechi dhidi ya Arsenal, lakini hilo bado halina uhakika.”
Cody Gakpo alianza kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool magharibi mwa London kuchukua nafasi ya Ekitike, akisaidiwa katika ushambuliaji na Dominik Szoboszlai pamoja na Florian Wirtz.
Liverpool walicheza bila mshambuliaji wa asili. Ekitike amefunga mabao manane katika mechi 18 za Ligi Kuu na ndiye mfungaji bora wa klabu hiyo katika mashindano yote.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Frankfurt alikuwa amefunga mabao matano katika mechi tano, lakini hakufunga katika mechi zake mbili za mwisho.