Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sita watajwa kumrithi Slot Liverpool

Muktasari:

  • Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool, saa 5:00 usiku wa leo itaikaribisha Galatasaray kwenye Uwanja wa Anfield katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kinachojadiliwa zaidi ni hatma ya kocha huyo raia wa Uholanzi.

LIVERPOOL, ENGLAND: HALI siyo hali Anfield na Kocha Arne Slot amekalia kuti kavu huku baadhi ya majina yakitajwa kuja kurithi mikoba yake kwa kile kinachoelezwa wakati wowote anapigwa chini Liverpool.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool, saa 5:00 usiku wa leo itaikaribisha Galatasaray kwenye Uwanja wa Anfield katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kinachojadiliwa zaidi ni hatma ya kocha huyo raia wa Uholanzi.

Inaelezwa kocha huyo aliyetua Liverpool tangu mwaka 2024, ameshindwa kuifanya timu hiyo kucheza soka la kuvutia na kupata matokeo mazuri, licha ya msimu uliopita ambao ndiyo ulikuwa wa kwanza kwake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England akiwa na kikosi hicho ambacho pia kilitumia karibu nusu bilioni kusuka kikosi, lakini mambo yamekuwa magumu na kushuka kiwango.

Uwezekano wa kocha huyo kufutwa kazi umeongezeka zaidi baada ya sare ya bao 1-1iliyoipata dhidi ya Tottenham Hotspurs, Jumapili iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu England na Dominik Szoboszlai aliitanguliza Majogoo hao wa Anfield kwa bao la dakika ya 18 kabla ya Richarlison kuisawazishia Spurs dakika ya 90.

Licha ya kuwa bado kuna baadhi ya mashabiki wanamuunga mkono, lakini presha inazidi kuwa kubwa na Daily Stars Sports limetaja majina ya makocha ambao yako mezani tayari kurithi mikoba yake kama Liverpool italazimika kufanya uamuzi mgumu wa kumtimua.


Xabi Alonso

Ndiye anayepigiwa chapuo zaidi. Kocha huyo, 44, kwa sasa hana timu baada ya kutimuliwa Real Madrid Januari, 2026. Aliwahi kuiongoza Bayer Leverkusen kushinda Bundesliga bila kupoteza mechi, pamoja na DFB Pokal na kufika fainali ya Europa League. Aliwahi pia kucheza Liverpool kwa miaka mitano, hivyo anaifahamu vizuri klabu hiyo. Hata hivyo, wakala wake amekanusha taarifa tayari kuna makubaliano ya yeye kuchukua nafasi hiyo.


Luis Enrique

Kocha wa PSG anayetajwa kuwa mmoja wa makocha bora duniani kwa sasa. Hata hivyo, uwezekano wa kuachana na PSG na kujiunga na Liverpool unaonekana kuwa mdogo, hasa kutokana na rasilimali kubwa ilizonazo timu hiyo ya Paris, Ufaransa.


Andoni Iraola

Chaguo la kuvutia kutoka Ligi Kuu England ni Andoni Iraola. Amefanya kazi nzuri Bournemouth licha ya changamoto nyingi anazokumbana nazo. Anaonekana kuwa na mashabiki wengi, lakini bado kuna maswali kama ana uzoefu wa kutosha kuiongoza Liverpool.


Julian Nagelsmann

Ni kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani mwenye mkataba hadi 2028. Ingawa bado anaweza kuondoka, Liverpool italazimika kuwa na uhakika mkubwa kabla ya kumchukua hasa kutokana na majukumu yake ya timu ya taifa.


Simone Inzaghi

Aliwahi kuiongoza Inter Milan kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2023 na mmoja wa makocha wanaoheshimika Italia.

Kwa sasa yupo Al Hilal ya Saudia Arabia ambano anapokea mshahara mkubwa, hivyo kurejea Ulaya inaonekana kuwa mbali.


Francesco Farioli

Ni jina jipya linalochipukia Ulaya baada ya kuiongoza FC Porto vizuri. Hata hivyo, akiwa na umri wa miaka 36, wengi wanaona kazi ya Liverpool inaweza kuwa kubwa sana kwake kwa sasa.