Vargas, Manzambi wang'ara, Uswisi ikimaliza makundi kibabe
Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya mwisho ya kundi B iliyopigwa kwenye Uwanja wa BC Place uliopo mjini Vancouver, Canada, ilianza kwa Uswisi kutawala kwa dakika 45 za kwanza, ingawa uimara wa wenyeji kwenye kuzuia mashambulizi ulisaidia kuipeleka mapumziko ikiwa salama.
VANCOUVER, CANADA: TIMU ya taifa ya Uswisi imemaliza hatua ya makundi ya Kombe la Dunia kwa staili ya aina yake, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo Canada na kumaliza vinara wa kundi B.
Katika mechi hiyo ya mwisho ya kundi B iliyopigwa kwenye Uwanja wa BC Place uliopo mjini Vancouver, Canada, ilianza kwa Uswisi kutawala kwa dakika 45 za kwanza, ingawa uimara wa wenyeji kwenye kuzuia mashambulizi ulisaidia kuipeleka mapumziko ikiwa salama.
Kipindi cha pili kilianza kwa Uswisi kuendelea kulishambulia lango la Canada, ambapo dakika ya 46, nyota wa timu hiyo, Ruben Vargas aliifungia bao la utangulizi akimalizia kazi nzuri ya kiungo wa kikosi hicho, Johan Manzambi.
Mfupa ukaendelea kuonekana mgumu kwa wenyeji Canada, baada ya dakika ya 57, kuruhusu bao la pili lililofungwa na Johan Manzambi akimalizia pasi ya mshambuliaji wa timu hiyo, Breel Embolo na kuihakikishia kumaliza vinara wa kundi hilo la B wakifikisha pointi saba.
Jitihada za wenyeji zikaonekana dakika ya 76, baada ya mshambuliaji wa timu hiyo, Promise David kuifungia Canada bao la kufutia machozi, akimalizia kazi nzuri ya kiungo, Nathan Saliba na kurejesha upya matumaini ya kikosi hicho japo hadi mwisho wa mechi hiyo kikosi hicho kikakubali kichapo cha mabao 2-1.
Matokeo hayo yanaifanya Uswisi kumaliza vinara wa kundi B na pointi saba, nyuma yake kuna Canada na Bosnia and Herzegovina zenye pointi nne kila moja, huku Qatar ikiwa mkiani na pointi moja baada ya timu zote kucheza mechi tatu za hatua ya makundi.
Historia ya Uswisi katika Kombe la Dunia ni ndefu na yenye mafanikio ya kawaida ambapo timu hiyo inashiriki mara 13 hadi sasa tangu ilipoanza pia kushiriki mwaka 1934, 1938, 1950, 1954, 1962, 1966, 1994, 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na 2026.
Katika Kombe la Dunia lililofanyika Ujerumani mwaka 2006, Uswisi ilitolewa katika hatua ya 16 bora bila ya kufungwa bao lolote katika muda wa kawaida, kwani ilitolewa kwa penalti 3-0 dhidi ya Ukraine baada ya suluhu ya (0–0) dakika 120.
Uswisi ilikuwa ni timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kuondolewa mashindanoni bila kufungwa bao hata moja kwa muda wa kawaida au nyongeza, ikiwa ni rekodi pia iliyotokea kwenye michuano hiyo iliyofanyika Ujerumani mwaka 2006.
Mbali na hilo, Uswisi iliandika rekodi mbovu pia kwani ilikuwa ni timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kushindwa kufunga hata penalti moja baada ya sare kwenye mechi ya mtoano, kufuatia kukosa zote tatu dhidi ya Ukraine.
Mafanikio makubwa kwa Uswisi ni kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia mara tatu, ikiwemo lililofanyika mwaka 1934, Italia, 1938 (Ufaransa) na 1954, ilipokuwa mwenyeji, ambapo haijawahi kufika nusu fainali wala fainali hadi sasa.
Kwa upande wa Canada ambao ni wenyeji wa Kombe la Dunia 2026, kwa kushirikiana na Marekani na Mexico, ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1986, ikiwa kundi moja na Ufaransa, Hungary na Soviet Union na kuchapwa mechi zote kisha kuishia hatua ya makundi.
Baada ya kutolewa hatua ya makundi mwaka 1986 huku ikiwa haijafunga bao lolote, timu hiyo ilichukua miaka 36, kufuzu tena Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar na kumaliza mkiani mwa kundi F, lililokuwa na Morocco, Croatia na Ubelgiji.
Alphonso Davies ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga bao la kwanza la Canada katika historia ya Kombe la Dunia, ambapo alifunga kwenye fainali za Qatar hatua ya makundi, wakati timu hiyo ilipochapwa na Croatia mabao 4-1, Novemba 27, 2022.
Hii ni mara ya tatu kwa Canada kushiriki Kombe la Dunia ikianza kwa mara ya kwanza mwaka 1986, kisha ikarudia tena 2022 baada ya miaka 36 na 2026, ikiwa mwenyeji na mara zote huko nyuma haijawahi kufika hatua yoyote ya mtoano ikikwamia makundi lakini safari hii imepenya 32 bora kutokana na kumaliza nafasi ya pili.