Sita hatarini Liverpool kisa Wirtz

Muktasari:
- Wirtz ameibuka kama moja ya mastaa ambao Liverpool inawahitaji baada ya kuvutiwa na kiwango bora alichoonyesha tangu msimu uliopita chini ya Xabi Alonso ambaye naye anaonekana kuwa katika mpango wa kutimkia Real Madrid.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL bado inaweza kujaribu kumjumuisha mmoja kati ya wachezaji wao sita kama sehemu ya ofa ili kuipata saini ya kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambaye timu yake inahitaji Pauni 126 milioni ili kumuuza.
Wirtz ameibuka kama moja ya mastaa ambao Liverpool inawahitaji baada ya kuvutiwa na kiwango bora alichoonyesha tangu msimu uliopita chini ya Xabi Alonso ambaye naye anaonekana kuwa katika mpango wa kutimkia Real Madrid.
Kumsajili Wirtz ni moja kati ya mambo ambayo kocha Arne Slot anayapigia hesabu ingawa kiasi cha pesa kinachohitajika kama ada ya uhamisho ndio kinawaumiza vichwa mabosi wa Liverpool.
Kwa mujibu wa Sky Sports, Liverpool inaweza kufanikisha dili hilo kwa gharama ndogo kuliko Pauni 126 milioni na hiyo ni kwa sababu inataka kumjumuisha mmoja kati ya wachezaji kama sehemu ya ofa.
Leverkusen, ambayo iko kwenye mazungumzo ya kumwajiri Erik ten Hag kuwa kocha mpya, inaripotiwa kuwa kwenye soko ikitafuta kipa, beki wa kati na mshambuliaji.
Kwa sababu hiyo Liverpool inataka kujumuisha mmoja kati ya mchezaji wa nafasi hizo kama sehemu ya dili la kumsajili Florian Wirtz ili kushusha gharama ya makuba-liano hayo hadi chini ya Pauni 115 milioni , ambayo ndiyo rekodi ya usajili nchini Uingereza iliyowekwa na Chelsea ilipomsajili Moises Caicedo katika dirisha la majira ya kiangazi ya mwaka 2023.
Bayer Leverkusen inadaiwa kuwa na nia ya kukamilisha makubaliano hayo haraka, huku ikielekea wazi kuwa Wirtz anatarajia kuondoka katika dirisha hili.
Mbali ya Wirtz, Liverpooli pia inakaribia kukamilisha usajili wa beki wa kulia wa Leverkusen, Jeremie Frimpong, ambaye anauzwa kwa Pauni 30 milioni.
Katika miezi ya hivi karibuni, Man City na Bayern Munich zimekuwa zikihusishwa na Wirtz lakini Man City ilijiondoa na staa huyu hakuwa tayari kuendelea kubakia Ujerumani, hivyo, Liverpool ilipogonga hodi akakubali kujiunga nayo lakini kwa sasa kinachoendelea ni majadiliano ya ada ya uhamisho.
Miongoni mwa wachezaji ambao Liverpool inaweza kuwatumia kama sehemu ya ofa ni pamoja na Caoimhin Kelleher, Joe Gomez, Darwin Nunez, Diogo Jota, Curtis Jones na Harvey Elliott.