Siri yafichuka sababu Haaland kuwekwa nje dhidi ya Madrid
Muktasari:
- Guardiola na vijana wake walisafiri hadi Bernabeu wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wao wa nyumbani wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya michuano hiyo kwa mabao 3-2.
MANCHESTER, ENGLAND: IMEFICHUKA Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola alimweka nje straika wake Erling Haaland katika mechi ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Jumatano usiku kwa kuhofia kutozidisha ukubwa wa jeraha lake baada ya kuonekana ameumia na kushindwa kuendelea mchezo wao wa mwisho dhidi ya Newcastle.
Guardiola na vijana wake walisafiri hadi Bernabeu wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wao wa nyumbani wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya michuano hiyo kwa mabao 3-2.
Haaland ndiye alifunga mabao yote mawili kwa upande wa Man City katika mechi hiyo lakini aliachwa benchi wakati wa mchezo wa mkondo wa pili uliopigwa Jumatano na Real Madrid kushinda mabao 3-1.
Uamuzi wa kumweka nje Haaland ulikuja siku chache baada ya Omar Marmoush ambaye ndiye alipangwa nafasi ya staa huyo katika mechi hiyo, kumvutia sana Guardiola baada ya kufunga hat-trick katika ushindi wao dhidi ya Newcastle.
Moja ya sababu zilizomfanya kocha huyo asimchezeshe Haaland ilikuwa ni utimamu wake wa kimwili kutokuwa sawa na ndiyo maana alifikia uamuzi wa kuanza na Marmoush badala yake.
Haaland ambaye aliripotiwa kupata majeraha na kushindwa kuendelea kwenye mchezo dhidi ya Newcastle alimpa wasiwasi kocha Guardiola ambaye baadae alithibitisha maumivu aliyopata hayakuwa makubwa sana na pengine angeweza kucheza mechi iliyopita.
Mchambuzi wa masuala ya michezo wa kituo cha TNT Sports, Rio Ferdinand alisema moja ya sababu zilizochangia Madrid kupata ushindi dhidi ya Man City ni kukosekana kwa Haaland.
"Kisaikolojia, unapoyaona majina ya wachezaji na kuona Haaland hayupo kwenye timu, kwanza kabisa mabeki wa kati na kipa watakuwa wakisema 'game on'. Itakuwa mechi rahisi, asilimia 100,"alisema Rio.