Siri ya vita za mapema England ni hii

Muktasari:
- Hii ni tofauti kabisa na ilivyokuwa mwaka jana baada ya ligi kumalizika ambapo ilichukua wiki tatu kabla ya timu kubwa za England kuanza usajili ambapo Tosin Adarabioyo alijiunga na Chelsea kama mchezaji huru, na Lucas Bergvall aliwasili Tottenham akitokea Djurgarden.
LONDON, ENGLAND: MAMBO ni mengi sana Ulaya. Wakati ligi zikiwa zimemalizika mwisho wa wiki hii, harakati mbalimbali zimeanza, kuna vigogo kama Manchester United wameshaanza maandalizi ya msimu na wengine wameshaanza usajili, yaani hakuna kupumzika.
Hii ni tofauti kabisa na ilivyokuwa mwaka jana baada ya ligi kumalizika ambapo ilichukua wiki tatu kabla ya timu kubwa za England kuanza usajili ambapo Tosin Adarabioyo alijiunga na Chelsea kama mchezaji huru, na Lucas Bergvall aliwasili Tottenham akitokea Djurgarden.
Mwaka huu licha ya dirisha la usajili kutofunguliwa, Manchester United imeripotiwa kuwa imeshafanya usajili wa Pauni 62.5 milioni kumchukua Matheus Cunha, wakati Liverpool ikiwa imekamilisha dili la Jeremie Frimpong na Florian Wirtz naye huenda akatua hapo.
Jambo la kwanza linaloonekana kuchangia vita hizi na pilika pilika za usajili mapema ni timu nyingi kutaka kuboresha maeneo yake ya ushambuliaji.
Kukosekana kwa mshambuliaji hatari lilikuwa sababu kuu ya Arsenal kushindwa kuendeleza mbio zao za ubingwa, pia Man United ilikuwa inakutana na tatizo sawa na hilo kama ilivyo kwa Chelsea na hata mabingwa Liverpool mashabiki wao walikuwa wakimlalamikia sana Darwin Nunez kwa kukosa ufanisi kwenye eneo la mwisho.
Timu zote hizi zinataka washambuliaji na idadi ya wale waliopo ni ndogo sana, mfano kwa straika wa Ipswich Town, Liam Delap anaonekana kufanya vizuri msimu uliomalizika hali inayosababisha Chelsea, Man United kutaka kumsajili.
Wakati huo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Viktor Gyokeres anayehusishwa na Arsenal naye bado anagombaniwa na Man United na Chelsea.
Timu zote hizo zinapambana kufanya makubaliano kwa haraka kwani zinaamini zikichelewa zinaweza kupigwa bao.
Hata hivyo, si suala la washambuliaji pekee timu nyingi zinapambana kutaka kuangusha utawala wa Man City na Liverpool ambao wamekuwa wakipotezana taji la Ligi Kuu England kwa karibia miaka saba, hivyo zimekuwa zikifanya usajili wa haraka ili kupata muda mwingi wa kujenga timu zao kabla ya msimu mpya wa ligi kuanza.