Siri imefichuaka! Andoni Iraola kutua Crystal Palace
Muktasari:
- ‘The Eagles’ inatafuta kocha mpya wa kuziba nafasi ya Oliver Glasner, ambaye anatarajiwa kuondoka Juni 2026 mkataba wake utakapomalizika.
LONDON, ENGLAND: RIPOTI za kushtukiza kutoka nchini Hispania zinadai kuwa, kocha wa Bournemouth, Andoni Iraola, yuko hatua za mwisho kujiunga na Crystal Palace, huku akitarajiwa kuondoka kwa "The Cherries" hivi karibuni.
Iraola (43) amekuwa akizivutia klabu kubwa za Ligi Kuu ya England ikiwemo Manchester United, Liverpool, Chelsea na Newcastle kutokana na kazi yake nzuri huko Vitality Stadium.
Hata hivyo, kituo cha habari cha El Chiringuito kimeripoti kuwa, kocha huyo raia wa Hispania amekaribia kufikia makubaliano na Palace.
‘The Eagles’ inatafuta kocha mpya wa kuziba nafasi ya Oliver Glasner, ambaye anatarajiwa kuondoka Juni 2026 mkataba wake utakapomalizika.
Inasemekana Palace imeweka mezani ofa nono ili kumshawishi Iraola kabla ya dirisha la usajili la majira ya joto kufunguliwa.
Ikiwa Palace itafanikiwa kumnasa Iraola, itakuwa ni ushindi mkubwa kwa klabu hiyo ambayo kwa sasa inapambana kwenye michuano ya UEFA Conference League kuwania kufuzu fainali. Hatua hiyo itaonyesha uthubutu mkubwa wa uongozi wa Palace kuwapiku matajiri wa EPL.
Hata hivyo, Man United ilikuwa ikimfuatilia Iraola tangu kufutwa kazi kwa Ruben Amorim, Januari 2026. Hata hivyo, United sasa inaonekana kumpa mkataba wa kudumu kocha wa muda, Michael Carrick, aliyefanikiwa kuivusha timu hiyo hadi kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa upande wa Liverpool, bado haijatoa uamuzi kuhusu hatima ya Arne Slot. Licha ya kushinda ubingwa wa EPL msimu uliopita, Slot amekuwa na wakati mgumu msimu huu licha ya kutumia pauni milioni 416 (Sh1.47 trilioni) kwenye usajili.
Chelsea nayo inaendelea kutafutaji kocha mpya baada ya msimu mbovu, huku kukiwa na wasiwasi juu ya usalama wa kazi hiyo chini ya wamiliki wa Clearlake ambao wameshafukuza makocha watano ndani ya miaka minne.
Crystal Palace pia ilikuwa ikihusishwa na kocha wa Villarreal, Marcelino, lakini vyanzo vinasema kipaumbele chao kikuu kwa sasa ni Iraola.
Iraola amekuwa lulu sokoni baada ya kuifanya Bournemouth kuwa timu tishio na inayocheza soka la kuvutia, jambo ambalo sasa linaonekana kumuweka kwenye ramani ya makocha wanaosubiriwa kwa hamu kuanza maisha mapya Selhurst Park.