Kwa nini Andoni Iraola anafaa EPL?
Muktasari:
- Mhispania huyo amefanya kazi ya ajabu katika timu hiyo iliyopo pwani ya kusini mwa England, akivunja rekodi ya pointi za Bournemouth katika ligi katika kila moja ya misimu yake miwili akiwa klabuni hapo tangu alipojiunga majira ya joto 2023, na kuna uwezekano mdogo atafanya hivyo tena msimu huu.
LONDON, ENGLAND: KUFUATIA habari kwamba kocha Andoni Iraola ataondoka Bournemouth baada ya mkataba wake kuisha, masikio mengi yamekuwa makini kote katika Ligi Kuu England kujua anakokwenda.
Mhispania huyo amefanya kazi ya ajabu katika timu hiyo iliyopo pwani ya kusini mwa England, akivunja rekodi ya pointi za Bournemouth katika ligi katika kila moja ya misimu yake miwili akiwa klabuni hapo tangu alipojiunga majira ya joto 2023, na kuna uwezekano mdogo atafanya hivyo tena msimu huu.
Iraola amejenga timu yenye uwezo wa kuwashinda walio bora zaidi huku ikicheza mtindo wa kusisimua, unaolenga kushambulia, wenye presha ya juu na unaoendeleza mtindo mpya wa soka ambao unapendeza machoni na pia una ufanisi.
Zaidi ya hayo, amefanikisha hayo wakati Bournemouth wamekuwa wakiuza mara kwa mara wachezaji bora. Majira ya joto yaliyopita pekee waliwapoteza mastaa wanne kati ya watano wa safu ya ulinzi ya kikosi cha kwanza, huku Dean Huijsen, Milos Kerkez na Illia Zabarnyi wote wakiondoka wakati Kepa Arrizabalaga alirudi kwenye klabu yake, Chelsea kabla ya kuuzwa Arsenal.
Mwaka uliotangulia mfungaji bora Dominic Solanke Januari iliyopita, mmoja wa wafungaji bora wa msimu huu, Antoine Semenyo, alihamia Manchester City. Cha kushangaza, Bournemouth hawaonekani kuwa dhaifu kutokana na hilo. Kufuatia ushindi uliostahili wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Arsenal ambao ulikuwa ni kipigo cha pili cha nyumbani kwa vinara wa ligi msimu huu, kikosi cha Iraola sasa kimefikisha michezo 12 ya Ligi Kuu England bila kufungwa. Huo ndio mfululizo mrefu zaidi wa kutopoteza kwa timu yoyote katika ligi hiyo wakati wowote msimu huu.
Mtindo wa uchezaji wa Bournemouth chini ya Iraola unastahili kwa Ligi Kuu England. Unajikita katika presha dhidi ya mpinzani na uchezaji wa haraka na wa kasi wanapopata mpira. Soka la Iraola, kulingana na mshindi mara sita wa Ligi Kuu England, kocha Pep Guardiola, ndilo hasa mwelekeo ambao soka linaelekea.
“Leo, soka la kisasa ni namna Bournemouth wanavyocheza, Newcastle wanavyocheza, Brighton wanavyocheza, Liverpool wamekuwa wakicheza hivyo siku zote,” anasema kocha huyo Manchester City.
Msimu wa 2024-25 ndio pekee uliorekodiwa Ligi Kuu England tangu 2006-07 ambao ulishuhudia mashuti mengi zaidi kutoka katika mashambulizi ya haraka (1.79 kwa kila mchezo) kuliko msimu huu (1.73). Idadi hiyo iliongezeka polepole kutoka 0.78 kwa kila mchezo katika msimu wa 2020-21 hadi zaidi ya mara mbili katika kila moja ya misimu miwili ya hivi karibuni.
Tangu Iraola alipotua England, ni Liverpool (148) na Chelsea (121), timu ambazo zinamiliki mpira kwa kiwango kikubwa na zina rasilimali nyingi zaidi, ndizo pekee zilizo na mashuti mengi zaidi kutokana na mashambulizi ya haraka katika michezo ya Ligi Kuu England kuliko Bournemouth (119), ambao pia wako nafasi ya tano kwa mabao kutokana na mashambulizi ya haraka, wakiwa na 18.
Katika kipindi hicho, wamekuwa wakishambulia kwa kasi zaidi kuliko timu nyingine, huku wastani wa kasi ya mashambulizi kuelekea mbele ukifikia mita 1.96 kwa sekunde. Ni timu nne tu ambazo zimekuwa na wastani wa pasi chache zaidi kwa kila mfululizo wa mchezo kuliko wao. Kiini cha falsafa ya Iraola ni kucheza kwenda mbele haraka iwezekanavyo.
“Jambo la kwanza tunalojaribu kufanya tunaporejesha mpira ni kumpa namba tisa. Kwa sababu huo ndio wakati ambao mpinzani huwa hajajipanga vizuri na unaweza kupata nafasi bora zaidi,” anaiambia Sky Sports katika mahojiano.
Kocha huyo anataka wachezaji wake pia kujaribu kushinda mipira ya juu uwanjani kabla ya kuunganisha kurejesha mpira na kushambulia haraka kuelekea golini. Katika kipindi chake akiwa Bournemouth, timu yake iko nafasi ya tano kwa kunyang’anya mpira juu (kushinda mpira ndani ya mita 40 kutoka lango la mpinzani), nafasi ya tatu kwa kunyang’anya mpira juu kunakoishia kuwa shuti, na nafasi ya nne kwa kunyang’anya kunakoishia kuwa bao. Vilevile ni timu tatu kati ya zilizo na kiwango cha chini zaidi cha pasi zinazoruhusiwa kwa kila kitendo cha ulinzi kuliko Bournemouth yake (10.5), jambo linaloonyesha kuwa wamekuwa moja ya timu zinazocheza kwa nguvu zaidi bila kumiliki mpira. Msimu huu, ni Liverpool (8) pekee waliopata mabao mengi zaidi kutokana na kunyang’anya mpira juu kuliko wao (6).
Baada ya mwanzo mgumu alipoondoka bila ushindi hata mchezo mmoja kati ya tisa ya kwanza akiwa kocha, na ilionekana kwamba alikuwa anaelekea kufukuzwa, alibadilisha hali kwa kiwango kikubwa. Tangu mwisho wa kipindi cha bila ushindi ni Arsenal, Manchester City, Liverpool, Aston Villa, Chelsea na Newcastle United pekee ambao wamekusanya pointi nyingi zaidi katika Ligi Kuu England kuliko Bournemouth (146, au wastani wa 1.47 kwa kila mchezo).
Inaweza kusemwa pia wamekuwa na bahati mbaya kutofanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki michuano ya soka Ulaya. Msimu uliopita, kwa mfano, Bournemouth walimaliza nafasi ya tisa. Takwimu za msingi zilionyesha walistahili nafasi ya Aston Villa katika Europa League.
Atakwenda wapi baadaye? Taarifa zinadai kwamba Iraola bado hajaamua hatua inayofuata. Haijulikani kama atataka kuingia moja kwa moja katika kazi nyingine majira yajayo ya joto, lakini hakuna shaka kwamba kutakuwa na shauku ya timu kubwa kumtaka.
Baadhi ya timu hizo zitatoka sehemu nyingine za Ulaya, huku Bayer Leverkusen na timu yake ya utotoni, Athletic Club, zikionekana kuwa na uwezekano huo, lakini kutokana na kutokuwa na uhakika mkubwa wa makocha katika Ligi Kuu England na mtindo wake wa soka kufaa zaidi ligi hiyo, kuna idadi kubwa ya klabu nchini England ambazo zinaweza kumuwania.
Baada ya kupanda ngazi kutoka kazi yake ya kwanza katika timu ya AEK Larnaca nchini Cyprus kwenda Mirandes ya Daraja la Pili Hispania, na kisha kuhamia Rayo Vallecano katika La Liga kabla ya kwenda Bournemouth, Iraola yupo katika mwelekeo wa kupanda. Inawezekana, atakuwa analenga kazi katika klabu kubwa zaidi kuliko Bournemouth baada ya hapo, ambapo hatalazimika kukabiliana sana na mauzo ya wachezaji.
Hata hivyo, pia kuna uwezekano kwamba klabu zitakuwa na wasiwasi kuchukua makocha ambao hawajawahi kumaliza juu zaidi ya nafasi ya tisa katika ligi yoyote. Kushindwa kwa Thomas Frank huko Tottenham Hotspur kunaweza kuzifanya klabu kusita kumpapatikia. Lakini, kazi ya Mhispania huyo Bournemouth bila shaka inavutia vya kutosha kwa mtu yeyote kumpa nafasi. Hizi hapa ni klabu tano za Ligi Kuu England ambazo zinaweza kumchukua.
LIVERPOOL
Kufuatia kipigo cha jumla cha mabao 4-0 dhidi ya PSG katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, matumaini pekee ya Liverpool kujiokoa msimu huu yapo katika kufuzu mashindano hayo msimu ujao. Mustakabali wa kocha mkuu Arne Slot uko shakani kutokana na hilo, ingawa alishinda ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka jana.
Wengi wanadhani kwamba kiungo wa zamani wa Liverpool, Xabi Alonso, angekuwa chaguo la kwanza kuchukua nafasi hiyo kwa kuwa pia hana kazi kwa sasa, lakini mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Richard Hughes, ndiye aliyemchukua Iraola kwenda Bournemouth, hivyo kuna angalau mtu mmoja katika nafasi muhimu Anfield anayempenda.
Mashabiki wa Liverpool wangefurahia soka lake la kasi, na timu tayari imejengwa kucheza kwa mtindo huo; ni Brentford (46) pekee walio na mashuti mengi zaidi kutokana na mashambulizi ya haraka katika Ligi Kuu England msimu huu kuliko wao (44), huku Liverpool wakiongoza ligi msimu huu kwa mabao yanayotokana na kunyang’anya mipira juu (8), kidogo mbele ya Bournemouth waliopo nafasi ya pili (6). Alonso angekuwa kikwazo pekee, ingawa kikubwa sana kwa Iraola kupata nafasi ya kazi Anfield.
CHELSEA
Liam Rosenior amekuwa Chelsea kwa miezi michache tu, lakini tayari kuna uvumi kuhusu mustakabali wake. Na wao ni aina ya klabu inayoweza kufanya mabadiliko ya kocha kwa sababu fursa wanayoipenda imejitokeza.
Wana kikosi chenye vijana wa moto kilichojaa vipaji vya kushambulia, na wachezaji wengi wanaoweza kuendana na mbinu za Iraola. Wana kiwango cha tatu cha chini zaidi cha kuruhusu pasi zinazofika kwa kila kitendo cha ulinzi Ligi Kuu England msimu huu (10.7, kidogo mbele ya Bournemouth wenye 11.0), huku ni Manchester City (54) pekee walio na matukio mengi zaidi ya kunyang’anya mpira juu yanayoishia kuwa mashuti kuliko wao (53). Hata hivyo, kuna uwezekano kwamba uzoefu wa klabu hiyo wa kumchukua Graham Potter kutoka Brighton unaweza kuwafanya Chelsea wasisite kuchukua kocha mwingine kutoka timu ya katikati ya msimamo katika Ligi Kuu England.
MANCHESTER UNITED
Michael Carrick kwa sasa ndiye anayeongoza mbio za kuwa kocha wa kudumu wa Manchester United baada ya mwanzo mzuri wa kipindi chake, lakini baada ya kipigo cha nyumbani dhidi ya Leeds, kuna uwezekano mkubwa hali inaweza kubadilika kati ya sasa na mwisho wa msimu, japo alikwenda kurekebisha katika ushindi wa bao 1-0 ugenini kwa Chelsea.
Iraola anaweza kuwa chaguo zuri kwa klabu ambayo imekuwa ikipenda kucheza kwa kushambulia moja kwa moja na haina uvumilivu mkubwa wa umiliki wa mpira wa taratibu. Hilo ndilo lililokuwa anguko la kocha aliyemtangulia Carrick, Ruben Amorim.
Carrick amejaribu kubadilisha hilo. Tangu achukue uongozi, ni Liverpool (29) na Bournemouth (26) pekee ambao wamekuwa na mashambulizi ya moja kwa moja zaidi na mfululizo wa mchezo unaoanzia ndani ya nusu yao na kusonga mbele angalau asilimia 50 kuelekea lango la mpinzani, ukimalizika kwa shuti au mguso ndani ya eneo la mpinzani kuliko United (25). Ni wazi wana wachezaji wa kumudu kwa mtindo huo. Haijulikani Iraola anawezaje kukabiliana na presha kuifundisha Old Trafford, kwa kuwa hajawahi kuifundisha klabu iliyo karibu kwa ukubwa wa United, na kuna hoja kwamba wanahitaji mtu mwenye uzoefu zaidi wa kiwango cha juu. Hata hivyo, anaweza kuwa chaguo la kuvutia kama wanataka kujaribu.
CRYSTAL PALACE
Taarifa zinaonyesha kwamba Crystal Palace walikuwa wakifikiria kumchukua Iraola, wakitaka awafanyie kazi inayofanana na ile aliyonayo Bournemouth. Palace wana kikosi kilichojengwa kushambulia kwa kasi na kimeonyesha ufanisi mkubwa katika hilo chini ya Oliver Glasner. Kina kasi kubwa zaidi ya wastani ya mashambulizi kuliko timu yoyote katika Ligi Kuu msimu huu (mita 2.04 kwa sekunde).
Kutakuwa na nafasi wazi Selhurst Park kwa kuwa Glasner tayari amethibitisha ataondoka mwishoni mwa msimu, lakini je, kazi hii itakuwa kubwa vya kutosha kwa Iraola? Je, itakuwa hatua ya juu kutoka Bournemouth?
NEWCASTLE UNITED
Hakuna mifano mingi ya makocha wanaohama kutoka klabu za katikati ya msimamo kwenda timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Newcastle United wanajivunia kuwa na mojawapo ya mifano iliyofanikiwa zaidi. Kipindi cha Eddie Howe hakijawa kizuri, lakini huenda kimekuwa kizuri vya kutosha kuwahamasisha wamiliki wa klabu hiyo kujaribu tena. Walimchukua Howe kutokana na kazi nzuri aliyofanya Bournemouth, na wanaweza kujaribu kurudia kwa Iraola. Mabadiliko ya haraka ya mashambulizi ni sehemu kubwa ya mchezo wa Newcastle, na kushambulia kwa kasi pia ni muhimu. Wanashambulia kwa wastani wa kasi sawa kabisa msimu huu na Bournemouth (mita 1.88 kwa sekunde), huku timu hizo mbili zikiwa nafasi ya tatu kwa pamoja katika kipengele hicho.
Kwa kuwepo uvumi mwingi kuhusu mustakabali wa Howe, chaguo hili linaweza kuwa na mantiki zaidi kuliko yote.