Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sio Man City tu, hata hawa wengine walipigwa

Muktasari:

  • Nottingham Forest ilifanikiwa kushinda mabao 7-0 dhidi ya Brighton wakati Man City ikicharazwa kwa mabao 5-1 na vijana wa Mikel Arteta, Arsenal.

LONDON, ENGLAND: WIKIENDI iliyopita ilikuwa na mambo mengi kwenye Ligi Kuu England. Moja kati ya vitu vilivyotokea vilikuwa ni vipigo vikubwa vilivyotokea katika mechi mbili.

Nottingham Forest ilifanikiwa kushinda mabao 7-0 dhidi ya Brighton wakati Man City ikicharazwa kwa mabao 5-1 na vijana wa Mikel Arteta, Arsenal.

Vipigo hivyo vimeendeleza kile kilichowahi kufanywa hapo awali ambapo baadhi ya timu pia ziliwahi kukutana na vichapo vikubwa. Hii hapa orodha ya mechi za ligi hiyo zilizowahi kushuhudia timu moja ikipokea vichapo vikubwa zaidi.


ARSENAL 5-1 MAN CITY-2024/25

Vijana wa Pep Guardiola waliendelea kuendeleza wimbi la matokeo mabaya msimu huu baada ya kichapo cha mabao 5-1, ambacho kilikuwa cha pili kwa ukubwa kwenye EPL tangu msimu uanze.

Katika mechi hiyo iliyopigwa dimba la Emirates, Arsenal ni kama ilikuwa inalipa kisasi cha kupigwa mabao mengi na mabingwa watetezi mwaka 2021 kwenye ligi hiyo. Katika mechi hiyo ya mwisho kuzalisha mabao mengi wakati timu hizo zilipokutana Man City ikiwa nyumbani ilishinda mabao 5-0.


ARSENAL 7-0 EVERTON-2004/05

Yalikuwa ni matokeo ya kushangaza katika msimu bora zaidi wa ligi kwa Everton. Matokeo hayo Everton iliyapata siku kadhaa kabla ya msimu wa 2004/05 kumalizika ikiwa ni siku chache  baada ya kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu uliofuata.

Ushindi huo ulikuwa mkubwa zaidi katika maisha ya ukocha ya Arsene Wenger akiwa kocha wa Arsenal wakati huo.

Kichapo hicho kilikuwa pigo kwa kikosi cha David Moyes katika msimu ambao kwa ujumla ulikuwa mzuri kwake na vijana wake na kwa wakati huo kilikuwa ni kipigo cha tatu kikubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.


C.PALACE 0-7 LIVERPOOL, 2019/20

Kichapo kikubwa zaidi kwa Crystal Palace katika historia ya Ligi Kuu kilitokea kwenye Uwanja wa Selhurst Park, walipofungwa 7-0 na Liverpool.

 Kipigo hicho kilikuwa cha kwanza kikubwa kwa Palace kuruhusu katika uwanja  wa nyumbani katika historia, na pia mara ya kwanza kwa Liverpool kushinda kwa tofauti ya mabao saba kwenye mchezo wa Ligi Kuu England katika historia.

Aibu ya Palace iliongezeka zaidi kutokana na ukweli kwamba Liverpool walikuwa hawajashinda mechi yoyote ya ugenini kwa zaidi ya mwezi mmoja.


LIVERPOOL 7-0 MAN UNITED-2022/23

Labda haya ndio matokeo ya aibu zaidi katika historia ya Ligi Kuu England kwenye miaka ya hivi karibuni. Manchester United ilikutana na usiku ambao haitausahau katika historia baada ya kichapo hicho kizito walichopata kwenye dimba la Anfield.

Kipigo hicho kilishtua kwa sababu Man United ilikuwa katika uelekeo mzuri chini ya Erik ten Hag na hapo ilikuwa imepita siku chache tu tangu kushinda Kombe la Carabao dhidi ya Newcastle United.

Mabao sita kati ya hayo yalifungwa kipindi chapili baada ya kile cha kwanza kumalizika kwa Liverpool kuongoza kupitia bao la  Cody Gakpo.


BLACKBURN 7-0 NOTTINGHAM-1994/95

Hadi sasa hicho ndicho kipigo kikubwa ambacho Nottingham Forest imewahi kupata katika historia ya Ligi Kuu England.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ewood Park, nyota wa Rovers, Alan Shearer ndiye aliwika sana akifunga hat-trick.


MAN UNITED 8-2 ARSENAL-2011/12

Hicho ndicho kilikuwa kipigo kikubwa zaidi kwa Arsenal kuwahi kukipata tangu 1927 ambapo ilikuwa imepita miaka 87 tangu ilipopoteza 7-0 mbele ya West Ham United.

Vilevile ilikuwa ndio mara ya pili kufungwa mabao manane katika mechi moja tangi 1896 ilipochapwa mabao 8-0 na Loughborough.

Katika mechi hii, Wayne Rooney ambaye ndiye alichukua tuzo ya mchezaji bora wa mchezo alifunga mabao mawili sawa na Ashley Young.


MIDDLESBROUGH 8-1 MAN CITY- 2007/08

Hayo yalikuwa moja ya matokeo mabaya zaidi katika kipindi kigumu cha Manchester City chini ya mmiliki wao wa zamani, Thaksin Shinawatra kabla ya kununuliwa na Waarabu.

Man City ilikutana na kipigo hicho mwishoni mwa msimu dhidi ya Middlesbrough ya Gareth Southgate. Licha ya kichapo hicho Man City ilianza msimu huo vizuri na ikamaliza hadi nusu ikiwa ndio inaongoza katika msimamo wa ligi.

Kwenye mechi hiyo kadi nyekundu ya mapema aliyopata Richard Dunne ilionekana ndio ilichangia sana Man City kufungwa mabao hayo kwani safu ya ulinzi ilikuwa ikicheza vibaya.


CHELSEA 8-0 ASTON VILLA-2011/ 12

Hicho ni kichapo kikubwa zaidi cha Aston Villa katika historia ya Ligi Kuu England na michuano yote kwa ujumla ambacho kilitokea mikononi mwa Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge kwenye msimu wa 2012/13.

Villa walikuwa wameingia kwenye mchezo huo wakionekana kurejea katika kiwango bora baada ya kuanza msimu kwa kutopoteza mechi sita mfululizo chini ya Paul Lambert, lakini walikutana na kitu cha tofauti kiasi cha kupokea kichapo hicho kizito ambacho kingeweza kuwa kikubwa zaidi kwani  Lucas Piazon alikosa penalti ya dakika za mwisho.


MAN UNITED 9-0 IPSWICH-1994/95

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Ipswich ndio ilikuwa imeibuka na ushindi lakini kisasi kilicholipwa dhidi yao kwenye uwanja wa Old Trafford kimebakia katika historia ya EPL hadi leo.

Huo ndio ulikuwa ushindi mkubwa zaidi kwa Sir Alex Ferguson kuwahi kuupata akiwa kama kocha.

Ipswich ilikutana na Man United yamoto iliyojaa mastaa lukuki waliokuwa bado vijana. Andy Cole alifanikiwa kufunga mabao matano peke yake katika mechi hiyo.

LIVERPOOL 9-0 AFC BOURNEMOUTH-2022/23

Ni kichapo kingine kikubwa kilichoshuhudiwa hivi karibuni kwenye Ligi Kuu England. Mchezo huo ambao ulipigwa katika dimba la Anfield uliiwezesha Liverpool kupata ushindi mkubwa zaidi katika historia ya ligi hiyo.

Pia iliifikia rekodi ya Chelsea mwaka 2012 kwa wachezaji saba kufunga kila mmoja katika mechi hiyo.

Bournemouth ilikuwa ndio imepanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza England pale ilipokuwa bingwa wa msimu wa  2021/22.



SOUTHAMPTON 0-9 LEICESTER-2019/20

Southampton iliwahi kuwa mhanga wa vipigo viwili vya aibu vya mabao 9-0 katika misimu miwili mfululizo (2019/20 na 2020/21).

 Hata hivyo, kilichoshtua zaidi kilikuwa ni kile cha kwanza ilichopokea katika uwanja wake wa nyumbani wa St. Mary’s kutoka kwa Leicester City, kwani ilikuwa mara ya kwanza kwa timu kufungwa mabao mengi kiasi hicho kwenye EPL baada ya miaka 24 kupita.


NOTTINGHAM 7-0 BRIGHTON-2024/25

Tangu kuanza kwa msimu huu Nottingham Forest inaonekana kuwa katika kiwango bora na hilo limejidhihirisha katika matokeo yake. Kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England na mechi hiyo dhidi ya Brighton iliyoonekana kuwa ngumu, iliendelea kudhihirisha kile ilichoanza nacho msimu huu. Chriss Wood ndiye aliibuka shujaa zaidi kwa Nottingham baada ya kutupia hat-trick.