Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sintofahamu mchezaji akiuawa kwa risasi Ghana

Muktasari:

  • Ingawa ni tukio la kwanza la kiharifu, lakini limesababishia wachezaji na mashabiki wa soka mshtuko katika kipindi hiki ambacho timu mbalimbali zinajipanga kwa ajili ya mechi za mwisho mwisho za Ligi Kuu Ghana.

ACCRA, GHANA: TUKIO la kuuawa kwa mchezaji wa Berekum Chelsea ya Ghana, Dominic Frimpong baada ya basi la timu hiyo kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa majambazi limeibua mjadala wa usalama kwa wachezaji nchini humo wanaposafiri kwenda na kutoka viwanjani.

Ingawa ni tukio la kwanza la kiharifu, lakini limesababishia wachezaji na mashabiki wa soka mshtuko katika kipindi hiki ambacho timu mbalimbali zinajipanga kwa ajili ya mechi za mwisho mwisho za Ligi Kuu Ghana.

Frimpong mwenye umri wa miaka 20 aliyejiunga na timu hiyo Januari, mwaka huu kwa mkopo akitokea Aduana FC aliuawa juzi baada ya watu wanaodaiwa kuwa majambazi wenye silaha kushambulia kwa risasi basi la timu yake.

Mchezaji huyo alikuwa akisafiri na timu wakirejea nyumbani baada ya mechi dhidi ya Samartex inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi. Berekum Chelsea iko nafasi ya tatu kutoka mwisho ikiwa na alama 35.

Kwa mujibu wa taarifa ya klabu, watu waliokuwa wamevaa barakoa wakiwa na bunduki za kivita walilivamia basi la timu hiyo baada ya kufunga barabara, kisha walianza kulifyatulia risasi za moto wakati wa wachezaji wakirejea nyumbani, ambapo moja ilipata mchezaji huyo kichwani. Haijafahamika washambuliaji hao walitaka nini katika tukio hilo, kwani hawakuchukua chochote isipokuwa walitokomea kusikojulikana.

Klabu hiyo iliongeza: “Walianza kulifyatulia risasi basi letu wakati dereva alipojaribu kurudi nyuma. (Baadhi ya) wachezaji na maofisa (wa timu) walikimbilia vichaka vilivyokuwa karibu kujinusuru.”

Jeshi la Polisi lilisema Frimpong alipata majeraha ya risasi na alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu, huku msako wa kuwatafuta watuhumiwa ukiendelea.

Polisi walisema wamepeleka askari zaidi na wataalamu wa kiuchunguzi katika eneo la tukio na kusisitiza kuwa “wahusika watakamatwa muda mfupi iwezekanavyo.”

Chama cha Soka Ghana (GFA), kilielezea kushtushwa na tukio hilo kikimtaja Frimpong kuwa mmoja wa vijana wenye vipaji vikubwa ambaye alikuwa akijituma uwanjani akiwa na mapenzi makubwa kwa klabu, huku ikivitaka vyombo vya usalama kuchukua hatua haraka za kiusalama.

GFA ilisema itapitia na kuimarisha mipango ya usalama kwa timu zinazokwenda kucheza mechi ili kukabiliana na matukio ya aina hiyo siku za usoni.

Mwandishi wa michezo nchini humo, Muftawu Abdulai, alikaririwa akisema tasnia ya michezo nchini humo imeghubikwa na mshtuko unaokatisha tamaa, akibainisha kuwa mashabiki wengi wanajiuliza kama ni salama kusafiri na kucheza mechi za ligi katika miji mbalimbali.

“Ikiwa maisha ya watu au wahusika wakuu wa mchezo hayawezi kulindwa, basi kucheza mchezo huo hakufai," alisema.

Frimpong amefariki dunia akiwa amecheza mechi 13 za Ligi Kuu Ghara msimu huu na kufunga mabao mawili.