Azam yaivunja rekodi ya Yanga, yakata tiketi ya fainali CRDB Cup
Muktasari:
- Bao la Mkongomani Jephte Kitambala katika dakika ya 113 ndio lililomaliza mechi hiyo huku Azam ikiwa pungufu baada ya dakika 90 za mechi hiyo kumaliza kwa sare ya mabao 2-2.
NDIO kama ulivyosikia hivyo matajiri wa Chamazi, Azam FC wametibua uwezekano wa kuwepo kwa dabi ya tano ya Kariakoo msimu huu baada ya kuifunga Yanga mabao 3-2, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jana, Jumapili
Bao la Mkongomani Jephte Kitambala katika dakika ya 113 ndio lililomaliza mechi hiyo huku Azam ikiwa pungufu baada ya dakika 90 za mechi hiyo kumaliza kwa sare ya mabao 2-2.
Ushindi huo, umeifanya Azam kumaliza unyonge mbele ya Yanga katika mechi ya tatu kukutana na timu hiyo katika michuano ya Kombe la CRDB.
Mara ya kwanza ilikuwa Juni 12, 2023 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ambapo Yanga ilishinda 1-0 kupitia bao la Mzambia Kennedy Musonda.
Timu hizo zilikutana tena katika fainali ya msimu wa 2023/24 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024. Baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 0-0, Yanga ilishinda kwa mikwaju ya penalti 6-5 na kutwaa ubingwa.
MPANGO WA IBENGE
Mpango wa kuanza na mshambuliaji mwenye kimo kirefu, Jean Kamanga Ngita (futi 6.5), uliisaidia Azam kushinda mipira mingi ya juu hasa katika nyakati ambazo Yanga ilifunga njia za mashambulizi ya pasi fupifupi.
Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Azam ilianza kwa kutafuta mianya katika maeneo mbalimbali ya uwanja huku ikimtegemea Idd Seleman 'Nado' na Feisal Salum katika ubunifu wa mashambulizi.
Pamoja na kutaka kujenga mashambulizi kwa pasi fupifupi, Azam ilibadilika mara kadhaa na kutumia mipira mirefu kutokana na faida ya urefu wa Ngita ambaye aliwazidi kimo mabeki wa kati wa Yanga.
Bakari Mwamnyeto (futi 6.1) alikuwa mchezaji mrefu zaidi katika safu ya ulinzi ya Yanga huku Ibrahim Hamad 'Bacca' akiwa na futi 5.9.
Hesabu za kocha Florent Ibenge zilijipa katika dakika ya 28 baada ya Pascal Msindo kupiga krosi iliyomkuta Ngita.
Mshambuliaji huyo aliudondoshea mpira kwa kichwa Himid Mao 'Ninja' ambaye naye alitumia kichwa kuupachika wavuni na kuipa Azam bao la kuongoza kabla ya mapumziko.
VITA YA VIUNGO
Moja ya maeneo yaliyokuwa na ushindani mkubwa katika mchezo huo ni kiungo ambapo kila timu ilipambana kuhakikisha inatawala umiliki wa mpira na mwelekeo wa mchezo.
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, alianza na Duke Abuya pamoja na Mudathir Yahya katika eneo la kati huku Allan Okello akiwa mbele yao kama kiungo mshambuliaji. Pembeni walikuwepo Pacome Zouzoua na Max Nzengeli.
Kwa upande wa Azam, Ibenge alianza na Himid Mao pamoja na Yahya Zayd katikati ya uwanja huku Feisal Salum akiwa mbele yao. Pembeni walicheza Ashraf Kibwe na Idd Seleman 'Nado'.
Eneo hilo ndilo lililoshuhudia vita kubwa zaidi. Baada ya Yanga kujikuta nyuma kwa bao moja, iliongeza kasi ya mchezo na kuanza kulimiliki zaidi eneo la kati. Hali hiyo ilionekana zaidi katika kipindi cha pili, hasa baada ya Azam kubaki na wachezaji 10 kufuatia kadi nyekundu.
YANGA ILIVYOBADILIKA
Baada ya kugundua mabeki wa Azam wakiongozwa na Yoro Diaby walikuwa wanakaba juu, Yanga ilifanya mabadiliko ya kimkakati kwa kumtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Depu ili kuongeza nguvu kwenye eneo la mwisho.
Mabadiliko hayo yaliifanya Yanga kuachana kwa kiasi fulani na mchezo wa pasi nyingi na badala yake kutumia mashambulizi ya moja kwa moja yakilenga kutumia mianya iliyokuwa ikiachwa na safu ya ulinzi ya Azam.
Depu alisimama karibu na Prince Dube katika eneo la ushambuliaji na kuifanya Yanga kuwa na nguvu zaidi ndani ya boksi la wapinzani.
Dakika ya 67, Yanga ilipata bao la kusawazisha kupitia Depu aliyefunga kwa kichwa baada ya mashambulizi ya mfululizo yaliyowalazimisha mabeki wa Azam kufanya kazi ya ziada.
Presha ya mashambulizi ya Yanga iliendelea kuiongezea Azam ugumu wa kucheza na ndipo dakika ya 69 Yoro Diaby alipolazimika kumchezea rafu Dube akiwa beki wa mwisho, jambo lililomfanya aonyeshwe kadi nyekundu ya moja kwa moja.
AZAM ILIIGOMEA YANGA
Licha ya kubaki pungufu, Azam haikukata tamaa. Ibenge alifanya mabadiliko ya haraka kwa kuwaingiza Lameck Lawi na Zidane Sereri ili kuimarisha eneo la kati na kuongeza nguvu katika kipindi kigumu cha mchezo.
Azam ilionyesha nidhamu kubwa ya kiuchezaji licha ya kucheza na mtu mmoja pungufu na ilifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 85, jambo lililoonekana kuwapa matumaini ya kutinga fainali.
Hata hivyo, furaha yao haikudumu kwa muda mrefu kwani Yanga ilisawazisha dakika tatu baadaye na kurejesha mchezo katika usawa.
Dakika 90 za kawaida zilipomalizika, timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 na hivyo mshindi kulazimika kupatikana katika dakika 30 za nyongeza.
VIKOSI VILIVYOANZA
Yanga: Djigui Diarra, Kibwana Shomary, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad 'Bacca', Duke Abuya, Mudathir Yahya, Allan Okello, Max Nzengeli, Pacome Zouzoua, Prince Dube.
Azam FC: Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Yoro Diaby, Twalib Mohamed, Pascal Msindo, Himid Mao, Yahya Zayd, Feisal Salum, Ashraf Kibwe, Idd Seleman, Jean Kamanga Ngita.