Morocco ilivyochezesha diaspora dhidi ya Brazil
Muktasari:
- Historia hiyo imeandikwa katika mechi yao ya hivi karibuni iliyomalizika kwa sare ya mabao 1-1 dhidi ya miamba ya soka duniani, Brazil na nyota pekee aliyezaliwa katika taifa hilo ni Azzedine Ounahi anayekipiga klabu ya Girona ya Hispania.
Timu ya taifa ya Morocco (Atlas Lions) imeandika rekodi ya kipekee na ya kihistoria katika fainali za Kombe la Dunia 2026, baada ya kuwa ya kwanza duniani kushusha kikosi cha kwanza (starting eleven) kilichoundwa na wachezaji 10 ambao hawakuzaliwa nchini mwao.
Historia hiyo imeandikwa katika mechi yao ya hivi karibuni iliyomalizika kwa sare ya mabao 1-1 dhidi ya miamba ya soka duniani, Brazil na nyota pekee aliyezaliwa katika taifa hilo ni Azzedine Ounahi anayekipiga klabu ya Girona ya Hispania.
Licha ya sare hiyo ya kiume dhidi ya mabingwa hao wa mara tano wa dunia, jambo lililoteka ni namna nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika ilivyokusanya vipaji vya "damu ya Morocco" vilivyozaliwa katika mataifa mbalimbali makubwa ya Ulaya na Amerika Kaskazini.
Mashujaa hao na walikozaliwa
Yassine Bounou ni mlinda mlango mkongwe na tegemeo alizaliwa mjini Montreal, Canada, kabla ya familia yake kurejea Morocco akiwa mtoto mdogo.
Noussair Mazraoui ni beki wa pembeni anayekipiga kwa kiwango cha juu Ulaya alizaliwa na kukulia Uholanzi, nchi inayofahamika kwa kulea vipaji vingi vya Kimorocco.
Beki Achraf Hakimi ambaye ni shujaa na nahodha wa Atlas Lions alizaliwa jijini Madrid, Hispania na alilelewa katika akademia ya Real Madrid kabla ya kuamua kuichezea Morocco katika ngazi ya kimataifa.
Chadi Riad beki huyu chipukizi na imara wa kati alizaliwa mjini Palma de Mallorca, Hispania, akitokea kwenye mfumo wa soka wa nchi hiyo.
Issa Diop beki huyu wa kati mwenye uzoefu mkubwa alizaliwa mjini Toulouse, Ufaransa, akiwa na asili mchanganyiko kabla ya kuchagua kuvaa jezi ya kijani na nyekundu ya Morocco.
Kiungo Neil El Aynaoui alizaliwa Ufaransa, akiwa ni mtoto wa nguli wa mchezo wa tenisi wa zamani wa Morocco, Younes El Aynaoui.
Ayyoub Bouaddi kiungo huyu fundi na mmoja wa chipukizi wanaotolewa macho na klabu kubwa alizaliwa pia kwenye ardhi ya Ufaransa.
Kiungo Ismael Saibari alizaliwa Terrassa, Hispania, akakulia Ubelgiji, lakini moyo wake ukachagua kuitumikia timu ya taifa ya wazazi wake.
Bilal El Khannouss kiungo mbunifu na mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho alizaliwa mjini Strombeek-Bever, nchini Ubelgiji.
Chemsdine Talbi winga huyu mwenye kasi na chenga za maudhi alizaliwa na kulelewa katika mfumo wa soka wa Ubelgiji.
Uamuzi wa Morocco kutumia wachezaji waliozaliwa nje ya nchi (Diaspora) si jambo la dharura, bali ni mkakati wa makusudi wa miaka mingi uliowekwa na Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF).
Nchi hiyo imeweka maskauti wengi Ulaya kufuatilia watoto wote wenye asili ya Morocco wanaochipukia kwenye akademia za Real Madrid, PSG, Ajax, na vilabu vya Ubelgiji.