Sinema nzima kufukuzwa kwa Ange ni hivi
Muktasari:
- Ripoti zinadai Forest tayari imeshawasiliana na kocha wa zamani wa Man City ambaye aliwahi kushinda taji la EPL, Roberto Mancini ili akawe kocha wao mpya.
NOTTINGHAM, ENGLAND: KOCHA raia wa Australia Ange Postecoglu anadaiwa kuwa alipewa taarifa ya kufutwa kazi akiwa njiani kuelekea katika vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kumalizika mchezo wao wa Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea na kupoteza kwa mabao 3-0.
Ripoti zinadai Forest tayari imeshawasiliana na kocha wa zamani wa Man City ambaye aliwahi kushinda taji la EPL, Roberto Mancini ili akawe kocha wao mpya.
Kipigo dhidi ya Chelsea kiliimfanya Postecoglou aendelee na mfululizo wa mechi nane bila ya kupata ushindi ikiwa ni siku 39 tangu achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Inaelezwa mmiliki wa Forest, Evangelos Marinakis, alifanya uamuzi wa kumfukuza kazi Postecoglu baada ya kipindi cha kwanza cha mechi yao dhidi ya Chelsea kumalizika.
Kwa mujibu wa tovuti ya TNT Sports, Postecoglou alionekana akiingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo lakini kabla hapo, aliripotiwa alishakuwa amepewa taarifa ya kufukuzwa mapema.
Baada ya kwenda katika vyumba hivyo alizungumza na wachezaji kisha alipita njia ambayo Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Edu Gaspar alikuwepo.
Postecoglou alionekana akiwa amebeba begi ambalo alienda nalo moja kwa moja kwenye eneo la maegesho ya magari ambapo baada ya kuingia katika gari lake alionekana akipiga picha na shabiki mmoja huku akitabasamu.
Dakika chache baadaye, habari ilienea kwamba alifutwa kazi jambo ambalo liliwashtua sana wachezaji wa timu hiyo.
Staa wa timu hiyo, Morgan Gibbs-White alifichua kuwa Ange alipoingia katika vyumba vya kubadilishia nguo hakuwaambia kabisa kama amefukuzwa na badala yake aliwaambia kwamba hapendezwi na matokeo pamoja na kukosa umakini ingawa alifurahishwa na namna walivyocheza.
Ripoti zinadai kwamba wachezaji wa Forest walikuwa na imani kwamba Postecoglou bado angeweza kubadilisha mambo.
Baada ya kuzungumza na kocha katika vyumba vya kubadilishia nguo, wachezaji wa Forest walienda katika mkutano na mabosi wa timu hiyo ambako walipewa taarifa ya kufukuzwa kwa Ange jambo ambalo liliwashtua.
Inaelezwa, Jumamosi hiyo hiyo baada ya mechi Forest iliwasiliana na Mancini na kumpa ofa ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa klabu yao.
Kocha huyu ambaye ni mshindi mara tatu wa Serie A na bingwa Ligi Kuu England mwaka 2012, amekuwa hana kazi kwa mwaka mmoja sasa tangu aachane na timu ya taifa ya Saudi Arabia.