Kumfukuza Amorim ni pesa nyingi
Muktasari:
- Mabosi wa Man United wanaendelea kumpa sapoti kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 licha ya kikosi kuanza msimu vibaya kwa mara ya kwanza tangu 1992.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United italazimika kumlipa Ruben Amorim pesa nyingi endapo itaamua kumfuta kazi kabla ya Novemba 1, imefichuka.
Mabosi wa Man United wanaendelea kumpa sapoti kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 licha ya kikosi kuanza msimu vibaya kwa mara ya kwanza tangu 1992.
Amorim aliteuliwa kuinoa Man United, Novemba Mosi mwaka jana akichukua mikoba ya Erik ten Hag na kocha wa muda, Ruud van Nistelrooy.
Kocha huyo Mreno alisaini mkataba wa miaka miwili na nusu akitokea Sporting Lisbon na analipwa mshahara wa Pauni 6.5 milioni kwa mwaka, huku mkataba ukiwa na kipengele cha kuongeza miezi 12. Na kinachoripotiwa ni kwamba ataweka mfukoni Pauni 12 milioni kama atafutwa kazi kabla ya kufikisha mwaka mmoja tangu alipokabidhiwa mikoba.
Wasaidizi wa Amorim kwenye benchi lake la ufundi nao watalazimika kulipwa fidia endapo Man United itaamua kuachana nao.
Tangu alipochukua mikoba timu hiyo imepata pointi chache Ligi Kuu England kuliko nyingine yoyote, ikivuna pointi 31 katika mechi 31.
Na wastani wa ushindi wa kocha huyo upo chini kuliko wa mwingine yeyote kwenye historia ya Man United tangu Vita vya Dunia vya Pili.
Lakini, mabosi wanaweza kuvumilia wiki saba zilizobaki kama wanahitaji kumfuta kazi ili kukwepa kumlipa pesa nyingi. Kikosi cha Man United kitakabiliana na Chelsea uwanjani Old Trafford katika mchezo wa Ligi Kuu England wikiendi na mechi zinazofuatia baada ya hapo ni kasheshe.
Itakuwa na mechi ya ugenini kukabiliana na Brentford kabla ya kukabiliana na Sunderland waliopo kwenye ubora mkubwa. Baada ya hapo, watakwenda Anfield kukabiliana na Liverpool kabla ya kukabiliana na timu ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu kwenye mechi kwa maana ya kufungwa mara nyingi na timu hiyo, Brighton, mechi itakayopigwa Old Trafford.
Novemba 1 itashuhudia Man United ikikipiga na Nottingham Forest, ambapo kocha mpya Ange Postecoglou, ambaye amekuwa na rekodi nzuri ya kuichapa Man United baada ya kushinda mechi tano alizokabiliana nayo alipokuwa Tottenham msimu uliopita.
Licha ya kwamba kocha Amorim hatima ya kibarua chake kikiwa hakijafahamika kama ataendelea kubaki Old Trafford hadi wakati huo, lakini mabosi wa Man United wanafikiria pesa ambayo watamlipa kocha huyo endapo kama wataamua kumfuta kazi kutokana na matokeo mabaya yataendelea kuiandama miamba hiyo.
Baadhi ya mastaa kwenye kikosi cha Man United wamepoteza imani na kocha Amorim, licha ya mabosi wa timu hiyo kukanusha jambo hilo. Kuna matumaini kwamba kuna baadhi ya vitu vimekuwa bora kwenye kikosi hicho cha Old Trafford msimu huu.
Kwa kulingana na rekodi zao za Ligi Kuu England msimu uliopita, Man United ilikuwa nafasi za chini kwenye rekodi za mashuti yaliyolenga goli, wastani wa uwezekano wa kufunga mabao, ambapo ilikuwa na wastani wa mashuti sita na pasi nane na miguso ya mipira kwenye boksi la timu pinzani.
Lakini msimu huu katika mechi nne ilizocheza za ligi, Man United inaongoza kwa mashuti na miguso ya mipira ndani ya boksi la timu pinzani, wakati ikiwa kwenye Tano Bora ya mashuti yaliyolenga goli, wastani wa uwezekano wa kupata bao na pasi kwenye boksi la wapinzani. Kinachowafanya watu waikosoe ni kushindwa kutupia mipira nyavuni, ambapo kikosi hicho kipo kwenye nafasi ya 11 kuhusu mabao na nafasi ya 17 kwenye uwezekano wa kufanya mashuti kuwa mabao.
Straika Benjamin Sesko atakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha anaifanya Man United inakuwa na rekodi bora kwenye hilo.
Sesko, 22, hakufanya mguso wowote ndani ya boksi la mpinzani katika miguso yake 20 aliyoifanya na alipiga shuti moja kwenye mechi nzima ya Manchester derby.
Beki wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand, 46, alisema: “Kitu kimoja kinachonipa wasiwasi ni Sesko. Hapewi nafasi za kutosha, hapewi huduma ya kutosha, hawamtengenezei nafasi.
“Hilo linanifikirisha. Straika mpya amekuja kwenye timu, unapaswa kumtengenezea nafasi.”