Bellingham aibeba England, ikitinga Nusu Fainali
Muktasari:
- England imelazimika Kutoka nyuma na kupata ushindi huo baada ya Norway kutangulia kufunga bao kupitia mshambuliaji Andreas Schjelderup katika dakika ya 36 akimalizia pasi ya kiungo na nahodha wake Martin Odegaard.
England imefanikiwa kutinga hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Dunia baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norway, shujaa akiwa yule yule kiungo Jude Belligham aliyeweka kamba mbili wavuni.
England imelazimika Kutoka nyuma na kupata ushindi huo baada ya Norway kutangulia kufunga bao kupitia mshambuliaji Andreas Schjelderup katika dakika ya 36 akimalizia pasi ya kiungo na nahodha wake Martin Odegaard.
Hata hivyo England ikafanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza kupitia Bellingham akimalizia pasi ya winga Anthony Gordon na kufanya timu hizo kwenda mapumziko mzani ukiwa sawa.
Kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa kushtukiza ambapo Norway iliweka mpira kimiani katika dakika ya 55 kupitia beki Torbjorn Heggem lakini likakataliwa na VAR na kufanya timu hizo kumaliza dakika 90 zikifungana bao 1-1.
Bellingham aliifungia England bao la pili katika dakika ya 93, akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Norway, Orjan Nyland kufuatia shuti la kiungo Morgan Rogers.
Bao hilo linakuwa la sita kwa Bellingham kwenye fainali zinazoendelea za Kombe la Dunia, akiendelea kuibeba England huku akiwa kiungo aliyefunga mabao mengi katika fainali hizo.
Dakika ya 99 England ilikaribia kupata mkwaju wa penalti lakini hata hivyo VAR ikapindua maamuzi hayo na mchezo huo kumalizika kwa dakika 120 kwa ushindi wa England wa mabao 2-1.