Shearer: Isak? Kama vipi aende
Muktasari:
- Shearer hapendezwi na hilo na ameitaka klabu yake ya zamani kumuuza tu Isak kama anataka kuondoka dirisha hili la usajili.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Newcastle United, Alan Shearer ameonyesha hasira zake juu ya mpango wa Liverpool kumsajili Alexander Isak baada ya kuchati kwenye grupu la WhatsApp ambalo yupo pia Gary Lineker.
Shearer hapendezwi na hilo na ameitaka klabu yake ya zamani kumuuza tu Isak kama anataka kuondoka dirisha hili la usajili.
Straika Isak, ambaye alifunga mabao 23 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita ameonyesha dhamira yake ya kutaka kuondoka Newcastle.
Hakuwamo kwenye kikosi katika mechi za pre-season huko Asia na alikwenda kufanya mazoezi katika klabu yake ya zamani ya Real Sociedad.
Liverpool chini ya kocha Arne Slot imepeleka ofa ya Pauni 110 milioni kwa ajili ya Isak, lakini Newcastle iligomea. Kinachovumishwa ni kwamba Newcastle inataka Pauni 150 milioni, lakini Shearer anaamini mshambuliaji huyo anapaswa kufunguliwa tu mlango wa kutokea, aondoke.
Kwenye kipindi cha redio mtandao cha The Rest Is Football, ambako Shearer alikuwa na Micah Richards na Lineker na gwiji huyo wa Newcastle alizungumza kwa uchungu kuhusu usajili wa dirisha hili.
“Tumeona hasira zako kwenye grupu letu wiki chache zilizopita,” alisema Lineker akimfanya Shearer kufunguka hisia zake bayana kuhusu dili la Isak.
“Nadhani hadi sasa dirisha limekuwa baya Newcastle,” alisema Shearer.
“Watapoteza wachezaji wao muhimu, mmoja wao ni fowadi bora kabisa kwenye ligi. Lakini, nipo sawa na hali ilivyo. Nilidhani angebaki walau hadi mwakani. Hali ilivyo, kama itashindikana, wamwambie tu, ‘Thank you’.”
Kuhusu ishu ya Isak, Shearer alisema hilo ni juu ya mchezaji huyo kuamua hatima yake.
Fowadi Isak ameshindwa kuhudhuria na wenzake kwenye mechi za pre-season huku akidaiwa kulazimisha mpango wake wa kwenda kujiunga na miamba ya soka ya Anfield na mabingwa wa England, Liverpool.