Shaun Bartlett aihimiza Bafana Bafana kumaliza ukame wa miaka 30
Muktasari:
- Amemalizia kwa kusema kuwa urefu wa wachezaji si kigezo kikubwa cha kufunga mabao, bali ni ubunifu na utofauti wa mbinu katika mipira ya adhabu ili kuwapa nafasi bora wachezaji muhimu kufunga.
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Shaun Bartlett, ameonesha imani kubwa kuwa Bafana Bafana inaweza kumaliza ukame wa kusubiri kwa miaka 30 kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), akisema kizazi cha sasa kina wachezaji wenye uwezo wa kuandika historia.
Afrika Kusini ilitwaa ubingwa wa AFCON mwaka 1996, lakini Bartlett anaamini mashindano ya mwaka huu yanayoendelea nchini Morocco yanatoa fursa adhimu kwa Bafana Bafana kuvuka hatua iliyofikia kwenye AFCON 2023 nchini Ivory Coast, ambako ilimaliza katika nafasi ya tatu.
Bafana Bafana imepangwa katika Kundi B pamoja na Misri, Angola na Zimbabwe, itaanza kampeni yake dhidi ya Angola baadae leo Jumatatu, Desemba 22, 2025 ikiwa na lengo la kupata mwanzo mzuri.
“Tuna nafasi nzuri ya kuandika upya historia kwa kikosi cha sasa, kwa sababu ni muda wa miaka 30 tangu tulipotwaa ubingwa wa AFCON. Fikiria kama timu yetu itaweza kwenda mbali na kushinda ubingwa baada ya miaka 30, hilo ndilo tumaini letu kubwa,” amesema Bartlett.
Bartlett amekiri kuwa mechi za mashindano makubwa kama AFCON huwa ngumu, lakini amesisitiza kuwa wachezaji wa sasa wanaelewa vyema kinachohitajika baada ya kufika hatua ya nusu fainali katika mashindano yaliyopita, hivyo amewahimiza kupambana na kufika fainali na ikiwezekana kutwaa ubingwa.
“Kiakili, hilo ndilo jambo ambalo kocha Hugo Broos amelifanyia kazi kwa kiwango kikubwa. Wachezaji wa sasa wana mtazamo imara zaidi na wamekuwa na uimara wa kisaikolojia kuliko hapo awali,” ameongeza.
Katika miaka ya hivi karibuni, Bafana Bafana imeonesha maendeleo makubwa chini ya kocha Broos, na Bartlett anaamini bado ina nafasi ya kufika mbali zaidi, akisisitiza umuhimu wa kuboresha mipira ya adhabu na kona (set plays), akisema ni silaha muhimu katika soka la kisasa.
“Ikiwa huwezi kufunga mabao kwa njia ya kawaida ya kuivunja safu ya ulinzi ya wapinzani, basi mipira ya adhabu imekuwa muhimu sana duniani kote, kwa kutumia mbinu tofauti kwenye set plays, tunaweza kuzishangaza timu kadhaa.” amesema.
Amemalizia kwa kusema kuwa urefu wa wachezaji si kigezo kikubwa cha kufunga mabao, bali ni ubunifu na utofauti wa mbinu katika mipira ya adhabu ili kuwapa nafasi bora wachezaji muhimu kufunga.