Shah Rukh Khan wa 20 duniani, namba moja India

MUMBAI, INDIA. KAMA unafuatilia filamu za Kihindi, jina Shah Rukh Khan. Wahindi wanamwita King Khan. Jabali haswa wa filamu za Kihindi.

Kama ilivyo kwa wanamichezo tasnia hiyo inawalipa vizuri, kwa Khan utajiri wake ni kwenye filamu, achana na vyanzo vingine ambavyo kwa staa maarufu yeyote lazima awe navyo kama dili za matangazo.

Khan mwenye umri wa miaka 57, ametoa filamu mpya 'Pathan' na imeendelea kumwongezea pesa na kwa sasa ni kati ya matajiri 20 duniani, huku nchini kwao akikamata namba moja.


ANAPIGAJE PESA

Anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 770 milioni.

Uigizaji ndiyo sehemu anakopiga pesa zaidi na kila kipande anachoigiza kinamwingizia pesa ndefu Dola 5 milioni na hujumuishwa pia kwenye mgao wa faida baada ya mauzo ya filamu.

Ana kampuni ijulikanayo kwa jina la Dreamz Unlimited inayomwingiza Dola 18 milioni kwa mwaka.

Ni mmoja wa wamiliki timu ya mpira wa Kriketi iitwayo Kolkata Knight Riders inayoshiriki Ligi Kuu ya mchezo huo maarufu nchini India sambamba na wamiliki wengine Juhi Chawla na Jay Mehta.

Pia ni balozi wa kampuni mbalimbali kubwa barani Asia na duniani kwa jumla, kama Hyundai, LG, Ambani’s Reliance Jio na Tata Group’s BigBasket na ni balozi wa utalii wa Dubai na zote hizo humwingizia zaidi ya Dola 30 hadi 40 milioni kwa mwaka mmoja.


NDINGA

Anamiliki ndinga kali zenye thamani kubwa ikiwemo Bugatti Veyron inayotajwa ni moja ya magari yenye spidi sana duniani na thamani yake ni Dola 1.2 milioni.

Pia anamiliki magari mengine kama;

SRK Car List

BMW 7Series Car

BMW 6 Series

Mitsubishi pajero

Audi A6

Land Cruiser

Rolls Royce Drophead Coupe

Magari hayo kwa jumla yana thamani ya Dola 4 milioni.


MJENGO

Yeye na mkewe Gauri Chibber wanamiliki mjengo wenye ukubwa wa mita za mraba 26,328 ulioko huko Mumbai na imepewa jina la Mannat. Khan na waliinunua mwaka 2001.

Pia ana mjengo wake mkali ulioko Palm Jumeirah huko Dubai, UAE na una vyumba sita vya kulala, Gym ma upo karibu na bahari. Pia anamiliki mijengo mingine New Delhi na London, Uingereza.


MSAADA KWA JAMII

Amekuwa akifanya kazi na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na The Make-A-Wish Foundation inayojihusisha na kutoa misaada ya matibabu kwa watoto wanaosumbuliwa na magonjwa makubwa yanayohitaji gharama kubwa kutibika.

Amekuwa mdau wa kudumu na shirika la Child Rights and You ambalo husaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu.

Aliwahi kutoa misaada kwa serikali na taaisisi mbalimbali zilizokuwa zinasaidia watu waliopatwa na virusi vya Corona.

Khan pia mwaka 2018 alianzisha taasisi aliyoiita Meer Foundation ambayo imekuwa ikisaidia wanawake na watoto waliounguzwa na moto ama tindikali.


BATA NA MAISHA BINAFSI

Alifunga ndoa na Gauri Oktoba 1991, baada ya miaka sita ya kuwa pamoja kwenye uchumba na wamefanikiwa kupata watoto watatu, wawili wa kiume, Aryan na AbRam na wa kike aitwaye Suhana ambaye kwa sasa anasomea masuala ya sanaa na uigizaji huko Marekani.