Sesko alivyoiokoa Man United dakika za jioni
Muktasari:
- Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa London, West Ham walionekana kuwa njiani kuchukua pointi tatu muhimu kufuatia bao la kipindi cha pili lililofungwa na Tomas Soucek, bao ambalo lingeisogeza timu hiyo karibu zaidi kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
Benjamin Sesko ameibuka shujaa wa Manchester United usiku wa jana baada ya kufunga bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi na kuiokoa timu yake ambayo ilionekana ipo hatarini kupoteza mchezo huo dhidi ya West Ham uliomalizika kwa sare ya 1-1.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa London, West Ham walionekana kuwa njiani kuchukua pointi tatu muhimu kufuatia bao la kipindi cha pili lililofungwa na Tomas Soucek, bao ambalo lingeisogeza timu hiyo karibu zaidi kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
Baada ya kipindi cha kwanza kilichokosa mvuto na kushuhudia nafasi chache za mabao, Manchester United walionekana kumiliki mpira zaidi bila kuwa na makali katika eneo la mwisho.
West Ham walipata bao lao baada ya makosa ya safu ya ulinzi ya United. Jarrod Bowen aliwahi mpira na kumpasia Soucek, ambaye alirudisha kwa Bowen kabla ya kupokea tena pasi na kupachika mpira wavuni. Hilo lilikuwa bao la tatu la Soucek dhidi ya United, na pia limemfanya kuwa mchezaji wa Czech mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England.
United walijaribu kurudi mchezoni kupitia bao la Casemiro, aliyefunga kwa kichwa kufuatia krosi nzuri ya Kobbie Mainoo, lakini VAR ilibaini kuwa kiungo huyo alikuwa tayari ameotea na bao likakataliwa.
Kocha Michael Carrick, ambaye amerejea kwa muda Old Trafford, alifanya mabadiliko muhimu kwa kumuingiza Sesko akitokea benchi ambaye baadaye aliinusuru United na kipigo dakika za mwisho.
Sesko alipachika bao hilo la kusawazisha kwa kumalizia mpira wa krosi iliyopigwa na Bryan Mbeumo. Hadi dakika 90 za mwamuzi zinamalizika, timu zote ziliondoka zikiwa zimegawana pointi.
Sare hiyo inakatisha mfululizo wa ushindi wa Carrick, lakini United bado inaendelea kubaki ndani ya nafasi nne za juu, huku matumaini ya kumaliza msimu kwa mafanikio yakiendelea kuishi.
Mechi nyingine zilizopigwa jana kwenye Ligi Kuu England, ilishuhudiwa Chelsea ikibanwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani na Leeds United baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Joao Pedro huku lingine likipachikwa na Cole Palmer kwa mkwaju wa penalti wakati mabao ya kusawazisha kwa upande wa Leeds yalifungwa na Lukas Nmecha huku lingine likifungwa na Noah Okafor.
Everton ikiwa nyumbani imekubari kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bournemouth sawa na Tottenham ambayo nayo imechapwa 2-1 na Newcastle United.
Leo tena Ligi hiyo itaendelea kwa michezo mitano ambapo Manchester City itawaharika Fulham, Sunderland watakuwa nyumbani dhidi ya Liverpool, Brighton watakuwa ugenini mbele ya Aston Villa, Crystal Palace wataikaribisha Burnley wakati Nottingham Forest itakuwa nyumbani dhidi ya Wolves.