Sergio Ramos apata timu Mexico
Muktasari:
- Gwiji huyo Mhispaniola amekwenda kujiunga na klabu ya Monterrey ya Mexico kwa mkataba wa miezi sita akiwa ni mchezaji huru.
MADRID, HISPANIA: BEKI wa mpira, Sergio Ramos ameripotiwa kushtua wengi kwa uhamisho wake wa kwenda Mexico bila ya mkewe mrembo Pilar Rubio.
Gwiji huyo Mhispaniola amekwenda kujiunga na klabu ya Monterrey ya Mexico kwa mkataba wa miezi sita akiwa ni mchezaji huru.
Ramos alikuwa hana timu yoyote tangu alipoachana na Sevilla kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.
Ramos, 38, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kwenye kikosi hicho cha Liga MX, Ijumaa iliyopita.
Ramas alifunga pingu za maisha na mrembo Pilar Rubio, ambaye ni mtangazaji maarufu wa televisheni na mwanamitindo wa Hispania mwaka 2019.
Wanandoa hao wamebahatika kuwa na watoto wanne - lakini mrembo Pilar ameripotiwa kugoma kufuatana na mumewe huko kwenye makazi mapya Mexico.
Kwa mujibu wa Bild, Rubio ataendelea kubaki Hispania wakati Ramos akienda zake kuishi Mexico kwa masuala ya kimpira.
Kinachoelezwa ni kwamba marafiki wa karibu wa mrembo Pilar, ndiyo waliofichua kwamba mwanamke huyo amechoka kuhamahama.
Ramos aliondoka Real Madrid kwenda kujiunga na Paris Saint Germain mwaka 2021 kabla ya kurudi tena LaLiga kujiunga na timu yake ya Sevilla mwaka 2023. Mrembo Pilar kwa sasa anaripotiwa kurudi zake kuishi Madrid mahali ambako amekuwa na mambo yake mengi ya kimaisha.
Mrembo Pilar alisema: "Safari hii sitaondoka, nimefanya hivyo mara mbili. Nibaki hapa Madrid, familia itabaki hapa na Sergio atakwenda peke yake."
Monterrey kwa sasa inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa LigaMX ikiwa imepata ushindi moja tu katika mechi sita za mwisho. Itacheza kwenye Kombe la Dunia la Klabu, ambalo litafanyika Marekani, Juni mwaka huu, ambapo itakwaana na Inter Milan, River Plate na Urawa Red Diamonds kwenye makundi.
Ramos atavaa jezi Namba 93 kwenye klabu hiyo ya Mexico.