Semenyo aitaka Man City fasta
Muktasari:
- Imeelezwa kwamba kwenye mkataba wa Semenyo, 25, kuna kipengele kinachotaja Pauni 65 milioni kuwa ndiyo pesa anayouzwa, ambapo kwa klabu itakayolipa pesa hiyo hadi kufikia Januari 10, itafanikiwa kunasa huduma yake.
LONDON, ENGLAND: WINGA machachari, Antoine Semenyo amesema anataka dili lake la kutua Manchester City likamilike kabla ya Januari 1.
Lakini, klabu yake ya Bournemouth ingependa kubaki na huduma ya mchezaji wao huyo kwenye mechi ngumu itakazocheza mwezi ujao.
Imeelezwa kwamba kwenye mkataba wa Semenyo, 25, kuna kipengele kinachotaja Pauni 65 milioni kuwa ndiyo pesa anayouzwa, ambapo kwa klabu itakayolipa pesa hiyo hadi kufikia Januari 10, itafanikiwa kunasa huduma yake.
Kiwango chake bora ndani ya uwanja msimu huu kimefanya timu nyingi kuhitaji saini ya mkali huyo wa kimataifa wa Ghana, ambapo Man City, Chelsea na Manchester United zote zimetajwa kuhitaji saini yake.
Semenyo matakwa yake ni kwenda kukipiga Etihad, hivyo hilo linaifanya Man City kuwa mstari wa mbele kwenye kuwania saini ya mchezaji huyo, ikisubiri dirisha la usajili lifunguliwe.
Ripoti zinadai kwamba Semenyo anataka mambo yote yafanyike kwa haraka ili awe mchezaji wa Man City wakati dirisha linafunguliwa Januari 1.
Lakini, Bournemouth inamtaka abaki hadi Januari 10, hiyo ikiwa na maana Semenyo acheze kwenye mechi dhidi ya Arsenal na Tottenham Hotspur kabla ya kutimiza ndoto zake za kwenda kujiunga na Manchester City.
Semenyo amefunga mabao tisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu, huku akifukuzia rekodi yake ya ubora kwa msimu katika kikosi hicho, ambapo alifunga mabao 11.