Sema su! mabosi PSG wakataa unyonge

PARIS, UFARANSA. UBAYA ubaya tu. Ikiwa Real Madrid itamchukua staa wa Paris Saint Germain Kylian Mbappe katika dirisha lijalo, mabosi wa PSG wamepanga kulipa kisasi kwa kuchukua baadhi ya mastaa tegemeo wa kikosi hicho ikiwa pamoja na Vinicius Jr, Rodrygo, Aurilen Tchouaméni, Eduardo Camavinga na Federico Valverde mwisho wa msimu huu.

Ishara zote zinaonyesha kwamba kuna asilimia nyingi za Madrid kumsajili Mbappe kama mchezaji huru katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwani fundi huyo amekataa kuurefusha mkataba wake na ameshawaambia viongozi wa PSG kwamba ataondoka mwisho wa msimu huu.

Imekuwa ni kawaida ya Real Madrid kuhusishwa na Mbappe kila mwaka laki ni kwa wakati huu mambo yanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kukamilika kutokana na mchezaji mwenyewe kuweka wazi mapema kwamba anataka kujiumnga na miamba hiyo ya Hispania.

Rais wa PSG Nasser Al-Khleifi  katika siku za hivi karibuni amefanya kila linalowezekana kuhakikisha Mbappe haondoki ifikapo mwisbo wa msimu huu lakini staa huyu ameshikilia msimamo wa kwamba ataondoka na hajabadilisha hadi sasa.

Ikiwa Mbappe ataamua kuondoka mwisho wa msimu huu kwa mujibu wa mkataba wake PSG haitopata chochote kwenye masuala ya ada ya uhamisho kwani ataondoka kama mchezaji huru.

Staa huyu wa kimatifa wa Ufaransa ambaye amejiunga na PSG mwaka 2017 amekuwa akiwindwa na Madrid kwa muda mrefu ambao wanaamini staa huyu ataenda kuwa mbadala sahihi wa  Cristiano Ronaldo na Karim Benzema kwenye eneo la ushambuliaji.

Inaelezwa kuwa  Al-Khelaifi amechukizwa sana na jinsi Madrid ilivyomshawishi Mbappe kiasi cha fundi huyo kugoma kusaini kipengele cha kuurefusha mkataba wake na kwa sababu hiyo anataka kulipa kisasi.

Tajiri huyo kutoka Qatar anadaiwa kutaka kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuhakikisha madili ya wachezaji wote waliotajwa hapo juu yanakamilika.

Hata hivyo bado inaonekana kuwa kazi ngumu sana kwani wachezaji wote hao ambao wanaonekana kuwa ndio kesho ya Madrid kwenye mikataba yao kuna vipengele vinavyozitaka timu zinazohitaji kuwanunua kutpa kiasi kisichopungua Euro 750 milioni kwa kila mmoja.

Huenda PSG ikatoa  pesa lakini sheria za usawa wa matumizi za FIFA zitakuwa zinawabana.PSG ilikuwa tayari kumuuza Mbappe katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi ambapo Al-Hilal ya Saudi Arabia ilikuwa tayari kumchukua na kutoa ada ya uhamisho isiyopungua Euro 200 milioni lakini Mbappe mwenyewe alikataa hata kukutana nao.