Saudi Arabia yavunja rekodi Kombe la Dunia

Doha, Qatar. TIMU ya Taifa ya Saudi Arabia imeanza vyema michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea huko Qatar baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Argertina.

Mchezo huo wa kundi C ulianza kwa Argentina kupata bao la utangulizi kupitia kwa nyota wake mahiri, Lionel Messi dakika ya 10 kwa mkwaju wa penalti kisha Saudia kusawazisha kupitia kwa Saleh Al-Shehri dakika ya 48 na Salem Al-Dawsari dakika ya 53.

Saudia inayoshika nafasi ya 51 kwenye viwango vya ubora Duniani imeivunjia rekodi ya Argentina ya kutokufungwa baada ya kucheza michezo 36 tangu mara ya mwisho miamba hiyo kufungwa na Brazili mabao 2-0 Julai 2019 hatua ya nusu fainali Copa Amerika.

Pia Argentina inapoteza mchezo wa Kombe la Dunia iliyoongoza kipindi cha kwanza kwa mara ya pili katika historia baada ya kutokea hivyo mwaka 1930 na Uruguay.

Hii ni mara ya pili kwa Argentina kupoteza mechi ya kwanza ya ufunguzi kufuatia mwaka 1990 kufungwa na Cameroon bao 1-0 ingawa ilifika fainali na kufungwa na Ujerumani Magharibi pia 1-0.