Santi Cazorla kulipwa kiduchu LaLiga
Muktasari:
- Staa huyo wa zamani wa Arsenal alirejea kwenye timu ya Oviedo mwaka 2023, ambako alicheza kwa kiwango bora msimu uliopita na kuisaidia timu hiyo kupanda ligi kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24.
MADRID, HISPANIA: KIUNGO fundi wa boli, Santi Cazorla amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea klabu yake ya ujanani Real Oviedo akiwa na umri wa miaka 40 na atalipwa mshahara mdogo zaidi kwenye La Liga.
Staa huyo wa zamani wa Arsenal alirejea kwenye timu ya Oviedo mwaka 2023, ambako alicheza kwa kiwango bora msimu uliopita na kuisaidia timu hiyo kupanda ligi kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24.
Alifunga kwa friikiki matata kwenye mechi ya mchujo ya nusu fainali La Liga 2 dhidi ya Almeria. Kisha alifunga penalti kwenye mechi ya marudiano ya fainali wakati walipoichapa CD Mirandes kwenye dakika za ziada.
Cazorla alijitolea kwenda kuichezea Oviedo — ambako alikuwa kwenye akademia yao kuanzia umri wa miaka sita hadi 16 — bure bila malipo yoyote, lakini kanuni za La Liga zinamhitaji walau kulipwa mshahara wa chini kabisa, ambao ni Pauni 77,000 kwa mwaka au Pauni 1,480 kwa wiki.
Kutokana na Oviedo kurejea kwenye La Liga, hivyo Carzola anaweza kukubali kulipwa mshahara wa chini zaidi ili kuitumikia timu ya mapenzi yake. Lakini, sasa mshahara wake utapaswa kuongezeka kwa Pauni 90,000 - kwa sababu kwenye La Loiga mshahara wa chini ni Pauni 168,000 kwa mwaka au Pauni 3,230 kwa wiki. Hiyo ina maana, mshahara anaolipwa Kylian Mbappe huko Real Madrid kwa wiki ni mkubwa mara tatu ya kiwango ambacho Cazorla atalipwa kwa mwaka na wote wapo ligi moja.
Na bado haitoshi, staa huyo atatoa asilimia 10 ya mshahara wake na mauzo ya jezi zake kwa akademia ya klabu hiyo ya Oviedo. Cazorla, ambaye atatimiza miaka 41, Desemba mwaka huu alifunga mabao matano na kuasisti matano katika mechi 35 alizocheza msimu uliopita.
Cazorla aliichezea Arsenal mechi 180 kwa kipindi cha miaka sita hadi 2018, lakini Oktoba 2016 alipata tatizo kwenye msuli wa mguu uliosababisha afanyie upasuaji mara 11. Tatizo lake lilikuwa kubwa kiasi cha kutishia kukatwa mguu, ambapo madaktari walimwambia si tu kucheza mpira, pengine hata kutembea asingeweza tena, hivyo apatwe kitu ambacho Cazorla alikatwaa na kufanyiwa upasuaji mwingine, ambao ulimlazimisha atolewe ngozi kwenye mkono wake ili kuwekwa kwenye jeraha.