Saliba halazimishi kuhama Arsenal

Muktasari:
- Mfaransa huyo amejipambanua kama moja ya mabeki wa kati bora kabisa wa Ulaya kutokana na kile anachokifanya Arsenal.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa kati, William Saliba hatalazimisha uhamisho wa kuachana na Arsenal dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi licha ya Real Madrid kuripotiwa kuhitaji saini yake.
Mfaransa huyo amejipambanua kama moja ya mabeki wa kati bora kabisa wa Ulaya kutokana na kile anachokifanya Arsenal.
Ataingia kwenye miaka miwili ya mwisho ya mkataba wake na hilo limeanza kuziamsha timu nyingine zinazotazamwa uwezekano wa kumchukua akakipige kwenye vikosi vyao.
Real Madrid ni klabu pekee ambayo inaweza kumng’oa Saliba kutoka Arsenal na rais wa miamba hiyo ya Bernabeu, Florentino Perez ni shabiki mkubwa wa beki huyo. Anahitaji kunasa saini ya Mfaransa akiamini atakwenda kuwa kiongozi kwenye safu ya ulinzi ya Real Madrid kwa miaka mingi.
Lakini, gazeti la L’Equipe linaripoti Saliba hawezi kulazimisha uhamisho wa kuondoka Arsenal ili kwenda Real Madrid na wakala wake watafanya mazungumzo na mabosi wa Arsenal kuongeza mkataba mpya, labla washindwane kwenye mshahara mpya.
Arsenal italazimika kumshawishi Saliba anashinda mataji akiwa kwenye kikosi hicho cha Londo Kaskazini. Mipango ya Arsenal kwa miaka ya karibuni ni kushinda mataji na hata mkurugenzi wa michezo, Andrea Berta hatakuwa tayari kumuuza Saliba kwenda Real Madrid au kwenye klabu nyingine yoyote.
Arteta aliulizwa kuhusu mipango ya Real Madrid juu ya beki wa kati Saliba, lakini alidai anaamini kwenye mazungumzo aliyofanya na beki huyo na kuwaachia wahusika, alisema: “Vitu vya aina hiyo nawaachia wahusika (mkurugenzi wa michezo wa Arsenal) Andrea (Berta) na klabu ndiyo izungumzie.”
Saliba mwenyewe alisema: “Kwa upande wangu, nina furaha sana kuwa mahali hapa. Nipo hapa miaka miwili na nusu. Hakuna tatizo, nina furaha na nataka kubaki hapa. Nataka kubeba mataji nikiwa na Arsenal. Ukiondoka kwenye klabu hii bila ya kushinda chochote, mashabiki watakusahau. Nataka kushinda kitu kikubwa hapa.”