Salah: Henderson aagwe kwa heshima Anfield
Muktasari:
- Salah alienda mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa mchango wa Henderson haukuishia uwanjani pekee, bali pia ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo ambapo alikuwa kiongozi halisi wa kikosi.
LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Mohamed Salah ameibuka na ombi maalumu kwa mashabiki wa Liverpool kuhakikisha wanampa aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Jordan Henderson, kwaheri ya heshima anayostahili atakaporejea katika Uwanja wa Anfield mwishoni mwa msimu huu.
Henderson anatarajiwa kucheza katika dimba hilo kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka ghafla mwaka 2023, wakati Liverpool itakapokutana na Brentford katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu England. Kuondoka kwake kwa haraka kulimnyima fursa ya kupewa heshima ya kuaga, tofauti na ilivyozoeleka kwa wachezaji waliotumikia klabu hiyo kwa muda mrefu.
Akizungumza na TNT Sports, Salah alisisitiza kuwa mchango wa Henderson ndani ya Liverpool haupaswi kusahaulika, akieleza wazi kuwa alikuwa mhimili muhimu wa mafanikio ya timu hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.
“Hakupata ile kwaheri aliyostahili kwa sababu aliondoka haraka. Watu wa jiji wanajua namna ilivyokuwa na maana kwake kuwa hapa kama nahodha kwa miaka 12,” amesema Salah.
“Natumaini mashabiki watafanya kitu cha kipekee kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa wa klabu hii.”
Salah alienda mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa mchango wa Henderson haukuishia uwanjani pekee, bali pia ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo ambapo alikuwa kiongozi halisi wa kikosi.
“Bila yeye na uwepo wake kwenye ‘dressing room’, tusingefanikisha mafanikio tuliyopata,” ameongeza Salah.
Kwa upande wake, Henderson aliwahi kueleza kuwa kuondoka Liverpool kulikuwa kama pigo kubwa kihisia, akifananisha hali hiyo na kuachana na kitu kilichokuwa sehemu ya maisha yake kwa muda mrefu.
“Kuondoka Liverpool ilikuwa ngumu sana, ilikuwa kama kuachana. Ilikuwa maisha yangu kwa muda mrefu, kisha ghafla ikaisha,” amesema Henderson.
“Kwa muda fulani nilishindwa hata kuangalia mechi, hasa za Liverpool.”
Mechi hiyo dhidi ya Brentford inatarajiwa kuwa na hisia kali kwa mashabiki, huku pia ikiashiria mwisho wa enzi muhimu ndani ya Liverpool. Pamoja na kurejea kwa Henderson, kuna dalili za mabadiliko makubwa kikosini hapo kuelekea dirisha la usajili wa majira ya kiangazi.
Hali hiyo inaifanya Liverpool kuwa katika kipindi cha mpito, ambapo wanapaswa kusawazisha kati ya kutoa heshima kwa mastaa wao wa zamani na kujenga kikosi kipya kitakachoweza kuendeleza mafanikio yao siku zijazo.