Salah aipa Liverpool matumaini
Muktasari:
- Taarifa hiyo inakuja baada ya Salah kupata majeraha ya misuli ya nyuma ya paja (hamstring) katika mechi dhidi ya Crystal Palace iliyomalizika kwa Liverpool kushinda mabao 3-1, wiki iliyopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL ina matumaini nyota wao Mohamed Salah atarejea uwanjani kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa hiyo inakuja baada ya Salah kupata majeraha ya misuli ya nyuma ya paja (hamstring) katika mechi dhidi ya Crystal Palace iliyomalizika kwa Liverpool kushinda mabao 3-1, wiki iliyopita.
Kulikuwa na hofu kuwa staa huyo wa kimataifa wa Misri huenda tayari amecheza mechi yake ya mwisho akiwa na Liverpool kutokana na majeraha aliyoyapata.
Hata hivyo, Liverpool walithibitisha Jumatano jeraha lake si kubwa na wanatarajia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 kurejea uwanjani kabla ya msimu kumalizika.
“Liverpool inathibitisha Mohamed Salah anatarajiwa kuwa fiti na kucheza tena kabla ya mwisho wa msimu huu,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Awali, mkurugenzi wa timu ya taifa ya Misri, Ibrahim Hassan, alidai Salah alipata majeraha makubwa ya kuchanika misuli ya paja, jambo ambalo lingemnyima nafasi ya kuaga mashabiki akiwa uwanjani.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot, pia alikiri kuwa kulikuwa na wasiwasi iwapo Salah angeicheza tena klabu hiyo.
“Hatuna uhakika. Hilo ndilo jibu sahihi kwa sasa,” alisema Slot.
“Huenda akarejea, lakini bado hatujui. Tunachojua ni msimu unaelekea mwisho ndani ya wiki nne au tano, hivyo hakuna mechi nyingi zilizobaki, tunasubiri kuona hali itakuwaje.”
Aliongeza Salah amekuwa akijitunza vyema kiafya katika miaka yote, hivyo anaamini muda wake wa kupona utakuwa mfupi.
Habari hiyo ni faraja kubwa kwa Liverpool katika harakati zao za kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwani kwa sasa, inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na tofauti ya pointi nane dhidi ya Brighton iliyopo nafasi ya sita.
Katika michezo yao iliyosalia, Liverpool itacheza ugenini dhidi ya Manchester United na Aston Villa, pamoja na kuzikaribisha Chelsea na Brentford kwenye viunga vya Anfield.