Saka tajiri mtoto, wala haringi

LONDON, ENGLAND. HIVI karibuni tovuti ya  Capology, ilitoa orodha ya mastaa wa England wenye utajiri mkubwa walioitwa timu ya taifa na mmoja wao ni Bukayo Saka ambaye hadi kufikia sasa anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Pauni 10 milioni.
Saka amewekeza pia kwenye biashara zinazomwingizia pesa na anatajwa atatajirika zaidi kutokana na soka na mambo mengine. Hata hivyo unajua anapigaje pesa.

ZINAKOTOKA PESA
Saka anapata pesa kutoka ndani na nje ya uwanja. Kwanza ni kupitia mshahara wake ambao unafikia Pauni 295,000 kwa wiki.
Pia ana biashara ya pilipili aliyoizindua katika siku za hivi karibuni ambayo inatarajiwa kumpa zaidi ya Pauni 2 milioni kwa mwaka.
Anapiga pesa za kutosha pia kupitia kampuni mbalimbali anazofanya nazo kazi. Kampuni ya kwanza ni New Balance ambayo inamlipa kwa kuvaa viatu vyao. Taarifa zinaeleza analipwa zaidi ya Pauni 1 milioni kwa mwaka kutokana na dili hilo.

Pia ana mikataba ya kuwa balozi na Kampuni za Amazon Prime, Fiverr, Beats na Call of Duty ambazo zote kwa pamoja zinampa zaidi ya Pauni 5 milioni kwa mwaka.


NDINGA
Ferrari 458 Spider
Mercedes Benz GLC-Class
Audi A8
Audi Q7
Range Rover


MSAADA KWA JAMII
Tangu mwaka 2022, Saka amekuwa akitoa pesa kuchangia taasisi ya Bigshoe inayojihusisha na kusaidia matibabu ya watoto kutoka nchi mbalimbali duniani.
Pia inaelezwa huchangia gharama za upasuaji kwa watoto 120 huko Kano, Nigeria.

NYUMBA
Alitumia  Pauni 2.3 milioni kununua nyumba London, England mwaka 2019 ambayo ndani yake ina eneo kubwa analolitumia kufanya mazoezi pale anapokuwa kwenye mapumziko.
Kwenye nyumba hiyo aliyoinunua akiwa anatimiza umri wa miaka 18,  pia anaishi na wazazi wake.


BATA NA MAHUSIANO
Kwa sasa yupo kwenye mahusiano na Tolami Benson ambaye amekuwa naye tangu mwaka 2020 na walikuwa wakifanya siri hadi siku za hivi karibuni na wamekuwa wakionekana pamoja sehemu mbalimbali.
Tolami anafanya kazi za mitindo na analipwa kwa kuwa modo wa kampuni mbalimbali.
Saka ni mmoja kati ya mastaa ambao hawapendi sana bata na muda wa mapumziko huwa anautumia kucheza game akiwa mwenyewe ama na ndugu zake.