Saha ataja viungo wawili wakunaswa Man United
Muktasari:
- Mshambuliaji wa zamani wa Man United, Louis Saha, ameishauri klabu hiyo kuwafikiria viungo wawili kama mbadala wa Casemiro, ambaye ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu wakati ambao dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
MANCHESTER, ENGLAND: MABOSI wa Manchester United wameambiwa wawasajili mastaa wawili hatari kama mbadala wa Casemiro, huku majina ya wachezaji watakaochukua nafasi ya Mbrazili huyo huko Old Trafford yakitajwa hadharani.
Mshambuliaji wa zamani wa Man United, Louis Saha, ameishauri klabu hiyo kuwafikiria viungo wawili kama mbadala wa Casemiro, ambaye ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu wakati ambao dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Mkataba wa Casemiro huko Old Trafford utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, baada ya tangazo kutolewa mwezi uliopita. Man United kwa sasa inahusishwa na viungo mbalimbali wanaoweza kujaza nafasi yake dirisha la usajili wa majira ya joto litakapofunguliwa.
Majina yaliyotajwa katika miezi ya karibuni ni pamoja na Carlos Baleba wa Brighton, Elliot Anderson wa Nottingham Forest na Adam Wharton wa Crystal Palace.
Katika wiki za hivi karibuni pia kumekuwa na tetesi kuhusu hali ya Sandro Tonali inayoendelea katika klabu yake ya Newcastle United, huku kiungo huyo wa Italia akihusishwa na Arsenal pia.
Saha ameeleza anaamini Tonali pamoja na mwenzake wa Newcastle, Bruno Guimaraes, wangekuwa sajili bora kwa kikosi cha Old Trafford. Katika mahojiano na AceOdds, alisema:
“Daima nimekuwa shabiki mkubwa na mtetezi wa Casemiro. Alipewa majukumu mengi mno katika miaka miwili iliyopita, lakini sasa jukumu lake limeeleweka na ametulia. Ameonyesha ni mchezaji wa kiwango cha dunia na ninaelewa kwa nini mashabiki wanataka abaki. Man United inahitaji ukali na mtu atakayedhibiti kiungo. Naona mtu kama Tonali au Guimaraes, ambao ni mastaa wawili hatari katikati ya uwanja.”
“Kuwa na wachezaji kama Kobbie Mainoo, unahitaji mtu mwenye uzoefu na maono atakayesaidia kusimamia mapito wakati Casemiro atapoondoka. Unahitaji uzoefu huo, uthubutu na uwezo wa kuongoza. Itakuwa vigumu kuchukua nafasi yake. Ukisajili mchezaji mchanga, kuna usumbufu fulani. Ni vizuri kwa siku zijazo, lakini pia unahitaji uzoefu. Kama Casemiro ataondoka, nafikiri mchanganyiko wa Wharton na Guimaraes utakuwa mzuri, kwa sababu Guimaraes ana sifa za nahodha.”