Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sancho ni bure, Dortmund, Galatasaray zatajwa

Muktasari:

  • Uamuzi huo unatokana na kushindwa kwa Sancho kurejea katika kiwango chake tangu aliposajiliwa kwa gharama kubwa na mashetani hao wekundu akitokea Borussia Dortmund mwaka 2024.

MANCHESTER United ipo tayari kuachana na winga wao wa kimataifa wa England, Jadon Sancho, 25, na kumruhusu aondoke bure mwisho wa msimu huu.

Uamuzi huo unatokana na kushindwa kwa Sancho kurejea katika kiwango chake tangu aliposajiliwa kwa gharama kubwa na mashetani hao wekundu akitokea Borussia Dortmund mwaka 2024.

Inaelezwa Man United ipo tayari kumruhusu staa huyu aondoke bila ya kudai chochote kwa sababu inahitaji kupunguza mzigo wa mishahara na kufungua nafasi ya kuwasajili wachezaji wapya.

Sancho ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Aston Villa, msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote, amefunga bao moja na kutoa asisti moja.

Kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji wanaokunja mshahara mnono Ligi Kuu England, akivuna takribani Pauni 300,000 kwa wiki.

Timu nyingi zinaonekana kutamani kumsajili ingawa itatakiwa akubali kupunguza mshahara wake pengine kufikia nusu au zaidi ya huo wa sasa.

Villa haionekani kuwa na mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu lakini kuna timu kadhaa kutoka Uturuki ikiwemo Galatasaray pamoja na timu yake ya zamani Dortmund, pia inamhitaji.


Marcus Rashford

MANCHESTER United inatajwa kujutia uamuzi wao wa kukubali kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa England, Marcus Rashford, 28, kwenda Barcelona kwa ada ya Pauni 26 milioni. Taarifa zinaeleza mabosi wa Old Trafford sasa wanaamini thamani halisi ya Rashford imepanda hadi kufikia takribani Pauni 50 milioni, kutokana na kiwango chake kizuri alichoonyesha msimu huu. Hali hiyo imewafanya United kuhisi waliingia mkataba wa haraka bila kutathmini vizuri soko, hasa ikizingatiwa kuna uhaba wa washambuliaji wenye ubora wa Rashford kwa sasa. Vilevile hiyo imewafanya kutohitaj kupunguza hata mia katika bei hiyo ya Pauni 26 milioni ambayo Barca inadaiwa kuomba kupunguziwa kidogo.


Marcos Senesi

BEKI wa kimataifa wa Argentina, Marcos Senesi, 28, anayeichezea Bournemouth, ameweka wazi nia yake ya kutaka kujiunga na Barcelona dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Senesi ameamua kutosaini mkataba mpya na Bournemouth, uamuzi unaofungua mlango wa mazungumzo ya uhamisho wake. Bournemouth imekubali kumuuza mwisho wa msimu huu kwa sababu mkataba wake wa sasa unamalizika Juni mwaka 2026, hivyo ikiendelea kumshikilia inaweza kujikuta ikimuuza kwa bei ya hasara au akaondoka bure.


Delap atafutwa kiangazi

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England, Liam Delap, 23, yuko mbioni kuondoka Chelsea mwishoni mwa msimu huu na tayari klabu kadhaa za Ligi Kuu England zimeonyesha nia ya kumsajili. Taarifa zinaeleza Manchester United, Newcastle United na Everton zinahitaji huduma ya mshambuliaji huyo kijana. Delap anahitaji muda zaidi wa kucheza tofauti na sasa katika kikosi cha Chelsea. Mabosi wa Chelsea wako tayari kusikiliza ofa na kumuuza ikiwa itapendezwa na dau litakalowekwa mezani.


Promise David

WEST HAM United inaongoza vita ya kuiwania saini yamshambuliaji wa kimataifa wa Canada, Promise David, 24, anayekipiga Union Saint-Gilloise. David amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu hali iliyowavutia mabosi wa West Ham ambao wamekuwa katika hali mbaya Ligi Kuu England kwa sasa. Inaripotiwa klabu hiyo ya London iko tayari kuingia kwenye mazungumzo rasmi mapema ili kuwapiku wapinzani wengine wanaomfuatilia straika huyo.


Morgan Rogers

TOTTENHAM Hotspur inajiandaa kutumia fedha nyingi dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kusuka kikosi chao kinachoonekana kuwa na hali mbaya msimu huu. Moja kati ya mastaa ambao Spurs imepanga kuwasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi ni kiungo wa kimataifa wa England, Morgan Rogers, 23, kutoka Aston Villa. Hata hivyo, Aston Villa hawaonekani kuwa tayari kumwachia kirahisi staa huyo na huenda wakahitaji ofa nono ili kumuuza.


Richarlison

TOTTENHAM Hotspur ipo tayari kusikiliza ofa na kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa Brazil, Richarlison, 28,  dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi. Richarlison ambaye hajawa katika kiwango chake bora hususan msimu huu kutokana na majeraha na ushindani mkubwa katika kikosi cha Spurs, ameripotiwa kuwa katika rada za vigogo wa wawili ambao ni Flamengo ya Brazil pamoja na Atletico Madrid ya Hispania. Ripoti zinaeleza Spurs hawamzuii kuondoka iwapo watapata dau linalofikia Pauni 45  milioni.


Luka Modric

AC MILAN ina imani kubwa kiungo wao wa kimataifa wa Croatia, Luka Modric, mwenye umri wa miaka 40, atasaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kusalia katika kikosi chao. Modric ambaye amekuwa akionesha kiwango cha juu licha ya umri wake, amekuwa kiungo muhimu katika kikosi cha Milan licha ya umri kumtupa mkono. Uongozi wa klabu umesema tayari umeanza mazungumzo na wakala wa Modric na kuna matumaini makubaliano yatafikiwa kabla ya kuanza kwa dirisha la usajili la majira ya kiangazi. Msimu huu Modric amecheza mechi 30 za michuano yote.