Rooney ampigia chapuo Keane Spurs
Muktasari:
- Tudor amepoteza mechi zote nne tangu achukue nafasi ya Thomas Frank mwezi uliopita.
IPSWICH, ENGLAND: KINACHOTAJWA kwa sasa huko England ni kwamba kibarua cha kocha wa muda wa Tottenham Hotspur, Igor Tudor kimeshikiliwa kwa nyuzi nyembamba ikidaiwa kwamba wakati wowote anaweza kutimuliwa kutokana na matokeo mabaya tangu alipotua kikosini wiki chache zilizopita.
Tudor amepoteza mechi zote nne tangu achukue nafasi ya Thomas Frank mwezi uliopita.
Lakini, wakati hilo likisikiliziwa kutokea, nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amepigiwa chapuo ya kwenda kuchukua mikoba katika kikosi cha Spurs, na kwamba atawanyoosha mastaa waliopo kutokana na tabia yake ukali.
Hayo ni maneno ya mshambuliaji wa zamani wa Man United, Wayne Rooney aliyedai kwamba Tottenham Hotspur wanahitaji kocha ambaye atawakazia na kuwabana wachezaji wao kwa kuwa wamekuwa wakionyesha ulegevu fulani bila sababu za msingi.
Rooney anaamini kuwa mtu mwenye haiba kama ya Keane anahitajika kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Spurs kwa sababu aliwahi kucheza naye ambapo ukali wake ulikuwa ukiwafanya wachezaji kuogopa na kupambania nembo ya Old Trafford bila kuchoka.
Akizungumza katika podikasti ya Stick to Football, Rooney alisema: “Wachezaji hao wanapaswa kujiangalia wenyewe. Kwa maoni yangu hawana aibu kabisa. Viwango vyao vya uchezaji, mtazamo wao, kukosa hamasa, kutopambania klabu, hakuna chochote ndani yao.”
“Wachezaji hao wanapaswa kujiangalia. Hii ni aibu. Nadhani wanahitaji mtu aingie kama Roy, na awatikise kweli. Wanahitaji kuwekewa hofu kidogo.”
Spurs kwa sasa iko kwenye mfululizo wa mechi 11 bila ushindi katika Ligi Kuu England, jambo linaloiweka kwenye hatari ya kushuka daraja, ikiwa pointi moja juu ya eneo la kushuka daraja, ikiwa na mechi tisa zilizobaki kuanzia kesho Jumapili itakapoifuata Liverpool.
Hali hiyo inatishia kuiweka katika hatari ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 49.
Wiki hii timu hiyo ilipoteza kwa mabao 5–2 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati akiwa mchezaji, Keane alijulikana kwa ukali uwanjani, akipata kadi nyekundu 12 katika maisha yake ya klabu na timu ya taifa. Baada ya kustaafu alifundisha Sunderland na Ipswich Town, lakini hajafundisha klabu yoyote tangu aondoke Ipswich miaka 15 iliyopita.
Kazi yake ya hivi karibuni ya ukocha ilikuwa 2019 alipokuwa msaidizi wa Martin O’Neill katika timu ya Nottingham Forest. Mkataba wa sasa wa Tudor na Spurs unaendelea hadi mwisho wa msimu, lakini kuna hisia kuwa ni lini ataondolewa.