Ronaldo, Messi mabilionea wapya mjini
Muktasari:
- Kwa mujibu wa jarida la Forbes, wawili hao ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakishindana katika kila kipengele cha mafanikio ya soka, sasa wamevuka kiwango cha utajiri wa zaidi ya Pauni 1 bilioni kila mmoja.
NEW YORK, MAREKANI: Nyota wawili waliotawala soka la dunia kwa zaidi ya miongo miwili, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, wameandika historia nyingine baada ya kufikia rasmi hadhi ya mabilionea kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia la 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, wawili hao ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakishindana katika kila kipengele cha mafanikio ya soka, sasa wamevuka kiwango cha utajiri wa zaidi ya Pauni 1 bilioni kila mmoja.
Messi, 38, amekusanya takribani Pauni 1.2 bilioni kutokana na mishahara na mikataba yake Barcelona, Paris Saint-Germain na Inter Miami.
Kwa upande wa Ronaldo, 41, mapato yake yameongezeka kwa kasi kubwa tangu alipojiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia mwaka 2023.
Mreno huyo alisaini mkataba unaokadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 178 milioni kwa mwaka pamoja na bonasi mbalimbali, jambo lililosababisha mapato yake ya soka kufikia takribani Pauni 1.26 bilioni.
Mbali na mishahara ya klabu, wawili hao wanaendelea kuvuna mamilioni kutokana na mikataba ya matangazo na biashara binafsi.
Ronaldo anaongoza kwa mapato ya nje ya uwanja kutokana na umaarufu wake mkubwa mitandaoni.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid anatajwa kuingiza karibu Pauni 48 milioni kwa mwaka kutokana na mitandao ya kijamii na mikataba na kampuni mbalimbali zikiwemo Nike na Herbalife pamoja na chapa yake ya CR7.
Messi ana mikataba mikubwa na Pepsi, Hard Rock pamoja na mkataba wa maisha na Adidas unaomuingizia karibu Pauni 44 milioni kwa mwaka.
Ripoti hiyo inaonyesha Ronaldo sasa ana utajiri wa takribani Pauni 1.4 bilioni, huku Messi akifikia pauni 1.2 bilioni.
Mafanikio hayo yanawaweka katika kundi maalumu la mastaa wachache wa soka waliofikia hadhi hiyo, wakiungana na gwiji wa England, David Beckham ambaye ameripotiwa kufikia kiwango hicho mwaka huu.
Licha ya mafanikio ya kifedha, macho ya dunia sasa yanaelekezwa kwenye Kombe la Dunia ambalo linaweza kuwa la mwisho kwa nyota hao wawili.
Kwa Messi, nafasi ipo ya kutetea taji alilolibeba mwaka 2022 nchini Qatar.
Kwa Ronaldo, mashindano hayo yanaonekana kuwa fursa ya mwisho kutimiza ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia ambalo ndilo taji pekee kubwa linalokosekana katika maisha yake ya soka.
Ureno itaanza kampeni yake dhidi ya DR Congo kabla ya kucheza na Uzbekistan na Colombia, huku Argentina ya Messi ikianza utetezi wa ubingwa dhidi ya Algeria kabla ya kukutana na Austria na Jordan.