Ronaldo ampa jeuri kocha Juventus
TURIN, ITALIA. KOCHA wa Juventus, Andrea Pirlo ameonekana kuwa na matumaini makubwa ya kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Italia maarufu kama Serie A kwa kuahidi kwamba watapambana hadi mwisho dhidi ya Inter Milan na AC Milan.
Usiku wa Jumatatu, Juventus iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Crotone. Aliyekuwa shujaa kwa upande wao kwenye mchezo huo alikuwa ni Cristiano Ronaldo aliyetupia mbili na kuisaidia timu hiyo kusogea hadi nafasi ya tatu.
Zimebaki pointi nane kwa Juventus wenye mchezo mmoja mkononi kuifikia Inter Milan ambao ndio vinara wa Ligi Kuu Italia wakiwa na pointi 53.
""Tulianza kuwa na wasiwasi kidogo, labda baada ya kufungwa mchezo wetu wa mwisho hicho ndicho kitu kilichochangia kuwa na wasiwasi, Lakini mabao tuliyofunga yalitusaidia na kutupa utulivu wa akili," amesema kocha huyo.
Kwa sasa Inter Milan wanaonekana kutawala mbio za ubingwa wa Serie A baada ya kuitwanga AC Milan siku chache zilizopita kwenye mchezo wa mahasimu 'Derby della Madonnina'.
"Ilikuwa mechi muhimu kwetu na jambo muhimu ni kwamba tumepata pointi tatu huku cha kuvuti hatukuruhusu bao," amesema kiungo wa timu hiyo, Aaron Ramsey.