Ronaldo, Al Nassr kizungumkuti

Muktasari:
- Mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or alitarajia kusaini mkataba mpya wa miaka miwili katika majira haya ya kiangazi, lakini mambo yamesimama kwa sasa.
RIYADH, SAUDI ARABIA: HATMA ya Cristiano Ronaldo katika kikosi cha Al Nassr inadaiwa kuwa iko shakani baada ya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kusitishwa kwa muda.
Mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or alitarajia kusaini mkataba mpya wa miaka miwili katika majira haya ya kiangazi, lakini mambo yamesimama kwa sasa.
Mkataba wa Ronaldo unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu lakini kwa mujibu wa tovuti ya Marca, mazungumzo ya kuongeza mkataba yamecheleweshwa kufuatia kiwango kibovu kilichoonyeshwa na Al Nassr msimu huu ambapo wamemaliza bila ya taji lolote.
Licha ya kufunga mabao 33 katika mechi 39 msimu huu, juhudi za Ronaldo hazijatosha kuiwezesha Al Nassr kushinda taji lolote kubwa.
Ripoti zinaeleza kuna uwezekano wa Ronaldo akahamia timu pinzani kama Al Hilal ambao tayari wamefuzu kucheza Kombe la Dunia la Klabu.
Al Nassr wamepoteza matumaini ya ubingwa na sasa wameshuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi baada ya kupoteza 3-2 dhidi ya vinara wa ligi Al-Ittihad, Jumatano.
Taarifa zinaeleza kuwa viongozi wa Al Nassr hawakupendezwa na tabia iliyoonyeshwa na Ronaldo baada ya kipigo hicho dhidi ya Al-Ittihad.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 40 aliondoka uwanjani kwa hasira na inadaiwa alirudi nyumbani akiwa bado amevaa jezi alizochezea mechi hiyo.
Kipigo hicho kilikuja wiki moja tu baada ya Al Nassr kutolewa kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Asia na timu ya Kawasaki kutoka Japan ambayo katika hatua ya fainali ilichapwa mabao 2-0 na Al-Ahli.
Mabosi wa Al Nassr na Ronaldo wote kwa sasa wanatafakari upya mustakabali wao ikiwa inafaa kuendelea kuwa pamoja au kila mmoja achukue upande wake.
Tangu Ronaldo ajiunge na Al Nassr 2023, klabu hiyo imemaliza nafasi ya pili katika misimu miwili mfululizo.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United anaweza kushawishika kukubali kujiunga na timu mpya ndani ya Saudi Arabia.
Licha ya mustakabali wake kuwa na sintofahamu, mtoto wake aitwaye, Cristiano Jr., amekuwa na wiki bora.
Jumanne iliyopita, Ronaldo Jr. anayechezea kikosi cha vijana cha Al Nassr aliteuliwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Ureno chini ya miaka 15.
Kupitia Instagram Ronaldo alionyesha furaha akiandika: “Ninajivunia sana wewe, mwanangu!”
Tangu ajiunge na Al Nassr mwaka 2023, Ronaldo ameshacheza mechi 103, akifunga mabao 91 na kutoa asisti 19.