Ronaldo achekwa, aibeba timu yake

Muktasari:
- Ronaldo, 40, aliingia kwenye mechi hiyo dhidi ya Denmark, akitambua timu yake ya Ureno ikiwa nyuma kwa bao 1-0, walilofungwa kwenye mechi ya kwanza na straika Hojlund, kipute hicho kilipofanyika jijini Copenhagen.
LISBON, URENO: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amepiga penalti ya hovyo huku mashabiki wakisema “Rasmus Hojlund amemvuruga kichwa.”
Ronaldo, 40, aliingia kwenye mechi hiyo dhidi ya Denmark, akitambua timu yake ya Ureno ikiwa nyuma kwa bao 1-0, walilofungwa kwenye mechi ya kwanza na straika Hojlund, kipute hicho kilipofanyika jijini Copenhagen.
Hojlund alipofunga kwenye mechi hiyo, alishangilia kwa kumuiga Ronaldo na staili yake ya “Siu”.
Kabla ya mechi ya marudiano ya Jumapili, CR7 wakati anazungumza na waandishi wa habari aliwataka mashabiki wa Ureno kuipa sapoti timu yao kwani itatinga nusu fainali ya michuano ya Nations League.
Lakini, fowadi huyo gwiji alipata nafasi mapema kabisa ya kuirudisha Ureno kwenye mstari katika mechi hiyo ya Lisbon, baada ya kupata penalti kwenye dakika ya tano tu ya mchezo.
Ronaldo, ambaye ameifungia Ureno mabao 135 kwenye soka la kimataifa alisogea mbele kupiga mkwaju huo wa penalti na alipiga hovyo na kipa wa Denmark, Kasper Schmeichel kuidaka bila ya shida yoyote, huku Ronaldo akibaki kwenye mshangao mkubwa kabla ya mashabiki wa Ureno kuanza kumrushia maneno.
Shabiki wa kwanza alisema: “Ile ni penalti mbovu kabisa niliyowahi kuishuhudia.”
Mwingine aliongeza: “Rasmus Hojlund amemvuruga kichwa Ronaldo.”
Shabiki mwingine alisema: “Wiki iliyopita Hojlund aligeuka Ronaldo, safari hii yeye amekuwa Hojlund.”
Shabiki wa nne alisema: “Kwa nini hakupiga kwa nguvu?”
Hata hivyo, Ronaldo aliisaidia timu yake kutinga nusu fainali ya Nations League baada ya kufunga mara moja katika ushindi wa mabao 5-2 na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-3 baada ya kuchezwa kwa dakika 120.
Ureno ilipata bao la kuongoza kwa Joachim Andersen kujifunga na kufanya matokeo kusomeka 1-1. Lakini, Denmark iliongeza bao jingine kupitia kwa Rasmus Kristensen kabla ya Ronaldo kusawazisha. Kiungo Christian Eriksen aliifunga tena kuipa faida Denmark, lakini Ureno ilisababisha mechi hiyo ikiingie kwenye dakika 30 za nyongeza kwa bao la Francisco Trincao. Kwa dakika hizo za nyongeza, Ureno ilifunga mara mbili na kupata ushindi huo mnono.