Ronaldinho abariki jezi namba 10 ya Yamal
Muktasari:
- Yamal alikabidhiwa jezi hiyo miezi michache iliyopita na kabla alikuwa anavalia namba 19. Pia aliwahi kuvaa jezi namba 27 baada ya kupandishwa kikosi cha wa kubwa na kwa cha vijana alianza na namba 41.
BRASILIA, BRAZIL: GWIJI wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho Gaucho ameunga mkono kitendo cha kinda wa Barcelona, Lamine Yamal kurithi jezi namba 10 ya Lionel Messi, akisisitiza dogo anastahili.
Yamal alikabidhiwa jezi hiyo miezi michache iliyopita na kabla alikuwa anavalia namba 19. Pia aliwahi kuvaa jezi namba 27 baada ya kupandishwa kikosi cha wa kubwa na kwa cha vijana alianza na namba 41.
Jezi hiyo imevaliwa na nyota wenye vipaji vikubwa Barcelona na kabla ya Messi aliivaa gwiji huyo ambaye aliondoka katika klabu hiyo baada ya kucheza misimu minne na Messi na kwa pamoja walicheza mechi 80 na kufunga mabao 67 kati ya 2004 na 2008 Dinho alipohamia AC Milan.
Baada ya hapo, Messi aliendeleza urithi huo na kuufanya kuwa wa kihistoria akifunga mabao 672 na kushinda mataji 35, na kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika uso wa dunia.
Baada ya Messi kuondoka Barcelona na kwenda PSG na sasa Inter Miami, jukumu hilo limechukuliwa na Yamal.
Licha ya umri wake mdogo, tayari anaonyesha uwezo mkubwa, kwani msimu huu chini ya kocha Hansi Flick, amecheza mechi 41 akifunga mabao 21 na kutoa asisti 5 katika mashindano yote.
Alipoulizwa kuhusu urithi wa jezi namba 10 na kama ipo katika mikono salama, Ronaldinho alisema: “Bila shaka. Lamine Yamal ni mmoja wa wachezaji bora duniani; bado ni mdogo sana, lakini tayari anafanya mambo ya ajabu. Jezi hiyo iko katika mikono salama kabisa.”
Pia alizungumzia hali ya sasa ya Barcelona akisema: “Bila shaka bado ni moja ya timu bora Ulaya, na huwa naifuatilia kila wakati nikitarajia icheze soka zuri.”
Hivyo basi, roho ya jezi namba 10 inaendelea kuishi Barcelona. Baada ya furaha na kumbukumbu zilizoachwa na Ronaldinho na Messi, sasa ni zamu ya Yamal kuendelea kuandika historia ya klabu.