Rodrygo kuzua vita kali England

Muktasari:
- Kutokana na hilo, mkali huyo wa Real Madrid, Rodrygo anaweza kuanzisha vita kali kutoka kwa klabu za Ligi Kuu England zitakazohitaji saini yake baada ya kuweka wazi kwamba yupo tayari kuachana na miamba ya Bernabeu.
MADRID, HISPANIA: STAA wa Kibrazili, Rodrygo yupo tayari kuachana na Real Madrid baada ya kuona anawekwa kando huku klabu hiyo ikionekana kuweka upendeleo kwa wachezaji Jude Bellingham na Kylian Mbappe.
Kutokana na hilo, mkali huyo wa Real Madrid, Rodrygo anaweza kuanzisha vita kali kutoka kwa klabu za Ligi Kuu England zitakazohitaji saini yake baada ya kuweka wazi kwamba yupo tayari kuachana na miamba ya Bernabeu.
Rodrygo ni mmoja wa mawinga bora kabisa duniani na amekuwa sehemu ya kikosi cha Madrid tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Santos mwaka 2019, akishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili. Lakini, kinachoelezwa aligomea kucheza mechi ya El Clasico ya Jumapili iliyopita wakati chama hilo linalonolewa na Mtaliano Carlo Ancelotti lilipokubali kuchapwa 4-3 na wapinzani wao, Barcelona.
Rodrygo anaripotiwa kwamba hafurahii jinsi ya hali ya mambo yanavyokwenda Real Madrid kwa sasa kwa sababu kumekuwa na upendeleo wa namba kwa wachezaji Bellingham na Mbappe, hivyo anafikiria kuachana na maisha ya Bernabeu kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Na sasa majaliwa ya Rodrygo kwenye kikosi hicho cha Real Madrid yatabaki mikononi mwa kocha mpya Xabi Alonso kama atahitaji kubaki naye na kumtafutia nafasi ya kucheza kwenye timu au ataamua kufungua tu milango wa Mbrazili huyo kuondoka.
Hatima ya Rodrygo hivyo ipo chini ya uamuzi wa Alonso, huku wakali wa mambo wakiamini Mhispaniola huyo anaweza kuchagua kuendelea na fowadi inayotumika kwa sasa, Bellingham, Mbappe na Vinicius Jr kama chaguo lake la kwanza.
Rodrygo amefunga mabao 68 katika mechi 267 alizocheza Madrid, lakini msimu huu amefunga mara sita na asisti tano tu kwenye mechi 22.