Robertson, Liverpool wamalizana England
Muktasari:
- Kwa sasa, changamoto ipo uwanjani, kwani wanakabiliwa na kazi nzito ya kugeuza matokeo dhidi ya PSG katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa huku pia wakipambana kulinda nafasi bora katika msimamo wa ligi.
LIVERPOOL, ENGLAND: HABARI hii inaweza kutafsiriwa tofauti na mashabiki wa Liverpool, kwani inaashiria mwisho wa enzi ya mmoja wa wachezaji muhimu zaidi kwa mafanikio ya hivi karibuni, Andy Robertson.
Robertson, ambaye ameitumikia klabu hiyo tangu aliposajiliwa kutoka Hull City 2017, anaondoka mwisho wa msimu huu akiacha alama isiyofutika, sambamba na Mohamed Salah ambaye tayari keshaaga.
Katika kipindi cha miaka tisa, amekuwa beki wa kushoto mwenye mchango mkubwa katika mafanikio ya Liverpool, akichangia timu kutwaa mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kuondoka kwake kunakuja muda mfupi baada ya taarifa kama hiyo kutoka kwa Salah jambo linaloonyesha kuwa Liverpool iko katika kipindi cha mpito, kwani wachezaji hao wamekuwa mhimili wa mafanikio ya klabu hiyo.
Licha ya kuwa na nafasi ya kuondoka Januari iliyopita kufuatia kuvutiwa na Tottenham Hotspur, Robertson aliamua kubaki kuitumikia Liverpool hadi mwisho wa mkataba wake.
Kwa sasa, changamoto ipo uwanjani, kwani wanakabiliwa na kazi nzito ya kugeuza matokeo dhidi ya PSG katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa huku pia wakipambana kulinda nafasi bora katika msimamo wa ligi.