Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cristiano Ronaldo atajwa bilionea wa kwanza mwanasoka

CR7 Pict

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa ya Bloomberg, wataalamu wa fedha walipiga hesabu za mapato yake yote katika kazi ya soka, uwekezaji wake pamoja na mikataba ya matangazo, kisha wakarekebisha kwa kuzingatia viwango vya sasa vya kodi na hali ya soko.

MSHAMBULIAJI nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ametangazwa kuwa mcheza soka wa kwanza duniani kufikia utajiri wa bilionea, baada ya thamani yake ya mali kukadiriwa kufikia pauni 1.04 bilioni (takribani Sh4.6 trilioni za Tanzania).

Kwa mujibu wa taarifa ya Bloomberg, wataalamu wa fedha wamepiga hesabu za mapato yake yote katika kazi ya soka, uwekezaji wake pamoja na mikataba ya matangazo, kisha wakarekebisha kwa kuzingatia viwango vya sasa vya kodi na hali ya soko.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mapato makubwa anayopata Saudi Arabia yamekuwa kama kifaa cha roketi kilichompeleka kileleni mwa orodha ya wanamichezo wanaoongoza kwa kipato duniani.

Ronaldo ndiye mchezaji wa kwanza wa soka kuorodheshwa katika Bloomberg Billionaires Index, na utajiri wake unadaiwa kumzidi kwa kiasi kikubwa mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi, ambaye kwa sasa anachezea Inter Miami nchini Marekani.

Mkataba wake wa maisha na kampuni ya Nike unakadiriwa kuwa na thamani ya pauni 745 milioni, ikiwa ndio dili lake kubwa zaidi la kibiashara. Pia ana ushirikiano na Tag Heuer, Armani, PokerStars, Samsung, Unilever, Louis Vuitton na kampuni nyingine nyingi.

CR 01

Kwa sasa Ronaldo anajenga nyumba ya kifahari nchini Ureno yenye thamani ya pauni 28 milioni, na mara nyingi huonekana akiwa amevalia saa na vito vya thamani kubwa duniani, ikiwamo Franck Muller Invisible Baguette Diamonds Imperial Tourbillon yenye thamani ya pauni milioni 1.13.

Mapato yake Saudi Arabia ni ya kushangaza. Anapata takribani pauni 300 kwa dakika akichezea klabu yake ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia, ambapo mkataba wake unamwingizia Pauni 167.9 milioni kwa mwaka. Hata hivyo, alikiri hivi karibuni kwamba angependa zaidi kucheza kwa ajili ya taifa lake la Ureno tu.

Mbali na mshahara wake mkubwa, Ronaldo pia anamiliki hisa katika klabu ya Al-Nassr, jambo linaloongeza zaidi utajiri wake.

Akipokea Tuzo ya Globo Prestigio kwa mchango wake mkubwa katika soka la Ureno, Ronaldo amesema: “Nimekuwa na timu ya taifa kwa miaka 22; hiyo peke yake inaonyesha mapenzi yangu kwa jezi hii, kwa kushinda mataji, na kwa kuchezea timu ya taifa. Kama ingekuwa inawezekana, ningependa kucheza mpira kwa ajili ya timu ya taifa pekee.”

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 40 bado yuko katika hali bora ya kimwili na anaendelea kufanya vizuri uwanjani.

“Nina mataji kadhaa nyumbani, lakini hili ni la kipekee. Nilijiuliza kama hii ni tuzo ya kumaliza kazi, nikapata wasiwasi, lakini siioni hivyo. Naichukulia kama mwendelezo wa kazi yangu yote,” ameongeza.

Ronaldo anaendelea kutumia sehemu ya utajiri wake kuwekeza kwenye miradi ya kifahari, ikiwamo jengo kubwa lenye ukubwa wa hospitali eneo la Quinta da Marinha, pwani ya Ureno, ingawa mradi huo umekawia zaidi ya miaka miwili kukamilika.

RONA 01

Nyumba hiyo inatarajiwa kuwa nyumba ya kifahari zaidi nchini Ureno, ikiwa na bwawa la kuogelea lenye njia ya chini ya maji na chumba kikuu cha kulala chenye ukubwa wa futi za mraba 1,000.

Mwaka 2024, Ronaldo aliuza ndege yake binafsi aina ya Gulfstream G200 aliyoinunua kwa pauni 16 milioni mwaka 2015, na kununua Bombardier Global Express 6500 mpya yenye thamani ya pauni 61 milioni.

Ndege hiyo nyeusi ina uwezo wa kubeba abiria 15, ikiwa na vyumba tofauti, sehemu ya kukaa yenye meza na sofa, chumba cha kulala chenye kitanda maradufu, na sehemu ya kuoga.

Aidha, Januari 2024, alinunua gari jipya la Ferrari Purosangue yenye thamani ya pauni 400,000, lakini bado siyo gari lake ghali zaidi.

Gari lake la kifahari zaidi ni Bugatti Centodieci adimu yenye thamani ya pauni milioni 8.5, na anadaiwa kuwa miongoni mwa watu 10 pekee duniani wanaomiliki gari hilo, lenye kasi ya hadi maili 236 kwa saa.

RONA 02

BADO ANANG'ARA UWANJANI

Licha ya maisha ya kifahari nje ya uwanja, utendaji wa Ronaldo bado uko juu. Hadi sasa msimu huu akiwa Saudi Arabia, amefunga mabao manne katika mechi nne.

Atakuwa akilenga kuendeleza kiwango hicho akiwa na timu ya Ureno chini ya kocha Roberto Martinez, katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Ireland na Hungary.

Ronaldo amesema bado ana ndoto ya kufikisha mabao 1,000 katika maisha yake ya soka (kwa sasa ana 946), lakini anasema kwa sasa hana presha kama zamani: “Nikiwa kijana nilikuwa na njaa sana ya mafanikio, nilitaka kula dunia nzima, lakini sasa najiona tofauti. Umri unatufundisha kutulia.”

Kwa sasa, Ronaldo anabaki kuwa mfano wa kipekee wa uthabiti, mafanikio na utajiri, akiwa mchezaji wa kwanza wa soka duniani kuingia katika orodha ya mabilionea na bado anaendelea kung’ara uwanjani.