Robert Lewandowski asubiri uchaguzi kuamua hatma yake
Muktasari:
- Uongozi mpya wa Barcelona unaweza kuamua kumpa mkataba mpya kwa masharti mapya au kuidhinisha kuondoka kwake ili kupunguza mzigo wa mishahara.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Poland, Robert Lewandowski, 37, ameamua kusubiri matokeo ya uchaguzi wa urais wa Barcelona unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao kabla ya kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake.
Lewandowski anahusishwa na ofa kadhaa zikiwemo AC Milan, Atletico Madrid, Chicago Fire, Fenerbahce, pamoja na Saudi Arabia.
Uongozi mpya wa Barcelona unaweza kuamua kumpa mkataba mpya kwa masharti mapya au kuidhinisha kuondoka kwake ili kupunguza mzigo wa mishahara.
Licha ya umri wake, Lewandowski bado anaamini ana uwezo wa kucheza soka la ushindani wa juu, hivyo kipaumbele chake cha kwanza kwa sasa ni kubaki Barca kabla ya kufikiria kuondoka.
Awali, iliripotiwa kwamba straika huyo angeachwa na Barca mwisho wa msimu huu kwa ajili ya kupunguza gharama za ulipaji mishahara na kupata nafasi ya kumsajili kwa mkataba wa moja kwa moja Marcus Rashford ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Nou Camp.
Mkataba wa Lewandowski unatarajiwa kumalizika ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Christian Pulisic
TOTTENHAM Hotspur imeonyesha nia ya kumsajili winga wa kimataifa wa Marekani na mchezaji wa zamani wa Chelsea, Christian Pulisic, 27, ambaye yupo tayari kurejea Ligi Kuu England akitokea AC Milan dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Pulisic ambaye ameonyesha kiwango bora akiwa na Milan anadaiwa kutaka kuondoka kupata changamoto mpya na wazo la kurudi England linaonekana kichwani mwake. Mkataba wa Pulisic unamalizika 2027.
Carlos Baleba
PSG ipo tayari kuingia vitani na Chelsea, Manchester United na Tottenham Hotspur kwa kuwasilisha ofa ya Pauni 100 milioni ili kumsajili kiungo wa Brighton na timu ya taifa ya Cameroon, Carlos Baleba, 22.
Baleba amekuwa miongoni mwa viungo wanaowindwa sana Ulaya, lakini Brighton haina presha ya kumuuza mapema.
Mara kadhaa imetajwa inahitaji Pauni 100 milioni ili kumuuza nyota huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Nick Woltemade
NEWCASTLE United ipo tayari kumuuza mshambuliaji Nick Woltemade katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kusajili straika mwingine.
Licha ya kuanza vizuri, hivi karibuni ameshindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa hali iliyosababisha vigogo wa timu hiyo kutaka kumuuza na kusajili mchezaji mwingine.
Newcastle inataka straika mwenye uwezo wa kufunga mabao kwani ndio kitu inachopata nacho tabu kwa sasa. Mkataba wa Woltemade unamalizika 2031.
Harry Maguire
MANCHESTER United inaamini itafikia makubaliano na beki wa kimataifa wa England, Harry Maguire, 32, na atasaini mkataba mpya utakaomuweka Old Trafford kwa muda mrefu zaidi.
Maguire amekuwa katika kiwango bora miezi ya karibuni, jambo lililosababisha benchi la ufundi kuwa na imani naye. Mazungumzo yanaendela na shida kubwa inaonekana kuwa masuala ya mshahara kwani Wekundu wanataka akubali kupunguziwa.
Pierre Kalulu
MANCHESTER United inataka kutuma maskauti Italia kwa ajili ya kumtazama staa wa Juventus, Pierre Kalulu atakayecheza mchezo kati ya Juventus na Inter Milan, leo Jumamosi, ili kukusanya taarifa zaidi za beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa.
Hata hivyo, mabosi wa Juventus hawapo tayari kumuuza kwa sasa ingawa hilo linaweza kutokea ikiwa ofa nono itawasilishwa. Mkataba wa Kalulu unamalizika 2029.
Aleksandar Stankovic
VIGOGO wa Ligi Kuu England ikiwa ni Manchester United, Arsenal, Chelsea na Tottenham Hotspur wanaendelea kumfuatilia kwa karibu kiungo wa Club Brugge na timu ya taifa ya Serbia, Aleksandar Stankovic, 20.
Mabosi wa Brugge wanahitaji zaidi ya Pauni 50 milioni ili kumuuza na wanafahamu itakuwa ngumu kumzuia kuondoka lakini kwa kiasi kikubwa cha pesa.
Santiago Castro
BOLOGNA imefikia makubaliano ya kumsainisha mkataba mpya mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Santiago Castro, 21, ambao utamwezesha kusalia kwa miaka minne na nusu na tetesi za kuhusishwa kwake na timu za kadhaa za Ligi Kuu England. Castro alikuwa akihitajika na Chelsea, Everton na Aston Villa, baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika Serie A. Straika huyo msimu huu amefunga mabao manane.