Rekodi ya Cristiano Ronaldo shangwe Colombia
Muktasari:
- Vijana wa kocha Roberto Martínez wapo Kundi K na itacheza mchezo wake wa kwanza Jumatano, Juni 17, dhidi ya DR Congo. Kisha watacheza dhidi ya Uzbekistan tarehe 23 kabla ya kufunga hatua ya makundi dhidi ya Colombia tarehe 27.
LISBON, URENO: Mkongwe Cristiano Ronaldo anajiandaa kuweka historia katika Kombe la Dunia 2026, itakayofanyika Marekani, Mexico na Canada, ambapo atacheza fainali zake za mwisho kwa mara sita, huku akipambana kuiletea Ureno taji hilo kwa mara ya kwanza.
Vijana wa kocha Roberto Martínez wapo Kundi K na itacheza mchezo wake wa kwanza Jumatano, Juni 17, dhidi ya DR Congo. Kisha watacheza dhidi ya Uzbekistan tarehe 23 kabla ya kufunga hatua ya makundi dhidi ya Colombia tarehe 27.
Hata hivyo, takwimu moja ya Kombe la Dunia inayomhusu nyota huyo wa Ureno inaweza kuipa Colombia matumaini ya kupata matokeo mazuri.
Mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 tayari yamezua mjadala mkubwa, hasa kuhusu mechi tatu za hatua ya makundi ambazo kila moja ya timu 48 itacheza. Na macho mengi sasa yanaelekezwa kwenye pambano la Ureno dhidi ya Colombia.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa kihistoria wa Bolavip kuhusu kiwango cha Cristiano katika Kombe la Dunia, mshambuliaji huyo amekuwa na ugumu kuonyesha ubora wake wa kiwango cha klabu katika hatua za mwisho za mashindano hayo, hasa anapokutana na timu za Amerika Kusini.
Kwa kweli, hakuna hata moja kati ya mabao yake manane ya Kombe la Dunia aliyofunga dhidi ya timu kutoka CONMEBOL (Shirikisho la Soka la Amerika Kusini). Cristiano amewahi kufunga dhidi ya Iran, Korea Kaskazini, Ghana, na Morocco, pamoja na mabao matatu dhidi ya Hispania katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia la Russia 2018.
Wakati huo huo, mechi zake dhidi ya timu za CONMEBOL zimekuwa chache, kwani amecheza michezo mitatu pekee dhidi ya timu za Amerika Kusini na hajafunga katika hata mmoja wao.
Mchezo wa kwanza ulikuwa sare ya 0-0 dhidi ya Brazil katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la Afrika Kusini 2010. Kisha ikafuata kipigo cha 2-1 dhidi ya Uruguay nchini Russia mwaka 2018, ambapo bao la Ureno lilifungwa na Pepe.
Katika mchezo wa marudiano dhidi ya Uruguay kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2022, Ureno walishinda 2-0, lakini mabao yote yalifungwa na Bruno Fernandes.
Ni muhimu pia kutambua kuwa nje ya mazingira ya Kombe la Dunia, Cristiano amewahi kufunga katika mechi za kirafiki dhidi ya timu kama Argentina na Ecuador.
Takwimu hii imeongeza matumaini kwa Colombia, ambao wanarejea kwenye Kombe la Dunia baada ya kukosa mashindano ya Russia 2018, huku wakielekea kwenye mashindano ya 2026 wakiwa na ndoto ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza wakiongozwa na nyota kama James Rodríguez na Luis Díaz.
Hata hivyo, Ureno pia wana ndoto hiyo hiyo, hivyo hawatakuwa tayari kujisalimisha kirahisi, hasa nahodha wao Ronaldo, ambaye anatarajia kutwaa taji ambalo amelifuata kwa mashindano matano yaliyopita.