Vinicius Jr, Mourinho kupiga kazi pamoja?
Muktasari:
- Kwa sasa ulimwengu wa soka sasa unasubiri kuona kama wawili hao wataelewana au wataingia kwenye mgogoro utakaoendeleza mtikisiko katika timu hiyo yenye historia kubwa pengine kuliko zote nchini Hispania na Ulaya kwa ujumla.
PORTO, URENO: ENZI mpya inaonekana kuanza Real Madrid huku Jose Mourinho akitajwa kurejea kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo, jambo ambalo litamuweka moja kwa moja katika chumba cha kubadilishia nguo pamoja na nyota wa timu, Vinícius Junior na Kylian Mbappe.
Kwa sasa ulimwengu wa soka sasa unasubiri kuona kama wawili hao wataelewana au wataingia kwenye mgogoro utakaoendeleza mtikisiko katika timu hiyo yenye historia kubwa pengine kuliko zote nchini Hispania na Ulaya kwa ujumla.
Baada ya msimu mbaya uliomalizika bila taji lolote, Real Madrid inaonekana kuwa na hitaji la sura mpya ya kocha. Hata hivyo, wengi hawakutarajia kurejea kwa Mourinho anayejulikana kama “The Special One” na kwa mitazamo yao Mourinho siyo chaguo bora kwa klabu ambayo tayari inaonekana kugubikwa na migawanyiko ya ndani.
Miaka miwili iliyopita Real Madrid ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Hispania (LaLiga) na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, imekuwa na mwenendo mbaya wa kinidhamu ambao umesababisha mambo kuwa mengi ndani ya muda mfupi, ikiachana na mmoja wa makocha bora wanaochipukia, Xabi Alonso na sasa Alvaro Arbeloa keshaaga kikosini.
Pia ngumi zimeripotiwa kupigwa kati ya mastaa wawili Federico Valverde na Aurélien Tchouameni. Si hivyo tu, lakini kuna vaibu flani la mashabiki ambalo limepungua, huku zomeazomea zikiwa nyingi.
Lakini, rais wa klabu hiyo, Florentino Perez anaripotiwa kumuona Mourinho kama mtu sahihi wa kuirejesha Real Madrid kwenye mafanikio, licha ya historia yake ya kauli kali, uamuzi wenye utata na mbinu zisizopendwa na baadhi ya mashabiki.
Historia ya mvutano kati ya Mourinho na Vinícius
Mafanikio yoyote ya Mourinho yatategemea mpango wake wa kuwa na maelewano na nyota wa timu hasa Vinicius Jr, ambaye aliripotiwa kuwa na mzozo wa wazi na kocha wa zamani, Alonso, katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2025-26.
Lakini hata kabla ya hapo, tayari kulikuwa na ishu yenye utata kati ya Mourinho na Vinícius, ambapo katika mchezo wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica mjini Lisbon, Vinicius alimshutumu winga wa Benfica, Gianluca Prestianni, kwa kumtolea maneno ya kibaguzi baada ya nyota huyo wa Real Madrid kufunga bao pekee la mchezo.
Vinicius alisema kauli hiyo ya kibaguzi ilitolewa huku Prestianni akifunika mdomo wake kwa jezi, tuhuma zilizoungwa mkono na wachezaji wenzake, Mbappe na Tchouameni. Hata hivyo, Prestianni alidai kuwa hakutoa tusi la kibaguzi bali tusi la ushoga, jambo ambalo baadaye lilimsababishia adhabu ya kufungiwa mechi sita na Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na lile la Dunia (Fifa).
Baada ya tukio hilo, Mourinho alimlaumu Vinícius kwa kuchochea hali hiyo kupitia namna alivyosherehekea bao lake, ambapo alisema: “Nilimwambia Vinícius unapofunga bao kama hilo, sherehekea kisha urudi katikati ya uwanja. Alipokuwa analalamikia ubaguzi wa rangi nilimkumbusha kuwa mtu mkubwa zaidi katika historia ya klabu hii (Eusebio) alikuwa mweusi. Klabu hii, kitu cha mwisho kabisa kuwa nacho ni ubaguzi wa rangi.”
Kauli hiyo ilipokewa kwa ukosoaji mkubwa, lakini Mourinho hakuwahi kuomba radhi wala kubadili msimamo wake waziwazi. Na sasa, miezi michache tu baadaye anatarajiwa kuwa kocha wa Vinícius Jr. Hata kama wawili hao wataweza kupita vyema katika tukio hilo, bado kuna changamoto nyingine kubwa, Vinicius siyo aina ya mchezaji anayependwa sana na Mourinho.
Kocha huyo wa Kireno hupendelea mawinga wanaofanya kazi kubwa ya kujilinda, wanaosaidia timu bila mpira na kufuata mfumo kwa nidhamu inayopita kiasi.
Kwa Vinícius mara nyingi yupo tofauti kabisa na hilo, ambapo nyota huyo hupendelea kucheza akiwa na mpira miguuni, hafanyi 'pressing' mara kwa mara wala kurudi kusaidia ulinzi. Pia ni mchezaji mwenye kujiamini sana, anayependa kutaniana na wapinzani na mashabiki baada ya kukokota mpira vizuri.
Zaidi ya hapo, Vinicius hana hofu ya kuingia kwenye migogoro na makocha, huku Mourinho naye akiwa kocha asiyevumulia hata tofauti ndogo ndani ya kikosi. Kwa kifupi, Valverde ndiye aina ya mchezaji ambaye Mourinho angependa sana kuwa naye kwani ni mwenye nidhamu, anayefanya kazi kubwa na mwenye kujitoa kwa timu tofauti kabisa na Vinícius.
Je, wanaweza kupiga kazi?
Licha ya dalili zote hatari, bado kuna uwezekano mkubwa wa Mourinho na Vinícius kufanya kazi vizuri pamoja na kupata mafanikio Real Madrid.
Kwa mujibu wa The Athletic, tayari kuna ishara nzuri kwamba Vinicius haoni ujio wa Mourinho kama tatizo kwake. Pia, mfumo anaoupenda Mourinho wa 4-2-3-1 au 4-3-3 unaweza kumfaa Vinicius hasa katika mashambulizi ya kushtukiza ambapo kasi, uwezo wa kukokota mpira na kutengeneza nafasi huonekana zaidi.
Jaribio kubwa litakuwa kuona kama Vinicius atakubali kujitolea zaidi kwa ajili ya mfumo wa Mourinho kama alivyofanya chini ya Carlo Ancelotti.
Ikiwa atafanya hivyo, anaweza kupata heshima kubwa kutoka kwa Mourinho.
Kwa upande mwingine, Mourinho atalazimika kuwa makini na kujifunza namna ya kumuongoza nyota mkubwa kama Vinicius.
Ni muda mrefu tangu Mourinho afanye kazi na mchezaji mwenye jina kubwa na kipaji kama hicho, na atalazimika kuepuka makosa yaliyosababisha tofauti zake za zamani na mastaa kama Iker Casillas, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo wakati wa kipindi chake cha kwanza Real Madrid.