Hat-trick za Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kwa ujumla ni takriban wachezaji 8,500 wamecheza mashindano hayo, lakini kumekuwapo na uhaba wa mastaa wanaofunga hat trick kukiwa na 54 hadi sasa.
WASHINGTON, MAREKANI: KUMEKUWAPO na mastaa wachache waliofunga mabao matatu (hat-trick), katika Kombe la Dunia tangu zilipoanzishwa fainali hizo 1930 nchini Uruguay, ikilinganishwa na umri wa miaka 106 wa mashindano hayo.
Kwa ujumla ni takriban wachezaji 8,500 wamecheza mashindano hayo, lakini kumekuwapo na uhaba wa mastaa wanaofunga hat trick kukiwa na 54 hadi sasa.
Hivi ndivyo ilivyo kuhusu hat-trick za Kombe la Dunia pamoja na orodha ya kila hat-trick iliyowahi kufungwa katika historia ya mashindano hayo.
MAAJABU YA SALENKO
Mrusi Oleg Salenko ndiye mchezaji pekee aliyewahi kufunga mabao matano katika mechi moja ya Kombe la Dunia aliyotupia wakati taifa lake lilipoichapa Cameroon 6-1 katika hatua ya makundi Juni 1994.
Mabao hayo yalifunika rekodi ya mshambuliaji wa Cameroon, Roger Milla ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao katika Kombe la Dunia.
Pia yalifanya jumla ya mabao ya Salenko katika Kombe la Dunia 1994 nchini Marekani kufikia sita baada ya kufunga pia dhidi ya Sweden katika hatua ya makundi.
Mabao hayo yalitosha kumpatia Kiatu cha Dhahabu cha mashindano hayo, ambacho alikigawana na gwiji wa Bulgaria, Hristo Stoichkov.
Ingawa mabao yake yaliisaidia Urusi kushinda, yalikuja kwa kuchelewa kwani tayari walikuwa wameondolewa kwenye mashindano hayo. Mechi dhidi ya Cameroon haikuwa na maana tena kwa sababu Sweden na Brazil tayari zilikuwa zimefuzu hatua ya 16 bora.
Salenko hakuwahi kuichezea tena Urusi, na mabao sita ya Kombe la Dunia 1994 ndiyo yalikuwa yake yote kwa timu ya taifa na baada ya hapo aliendelea kuichezea kisha akastaafu.
HAT-TRICK YA HARAKA
Hat-Trick ya haraka zaidi katika historia ya Kombe la Dunia ilifungwa na Erich Probst Juni 1954, ambapo Muastria huyo alitupia ndani ya dakika 24 za mwanzo katika mechi ya hatua ya makundi dhidi ya Czechoslovakia na kuifanya Austria iongoze 4-0 mapema tu.
Baada ya Ernst Stojaspal kufunga bao la kwanza dakika ya tatu, Probst aliongeza mengine dakika ya nne, 21 na 24 na kuweka rekodi ya hat-trick ya mapema zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Hata hivyo, hiyo haikuwa hat-trick ya haraka zaidi kwa muda uliotumika kati ya bao la kwanza na la tatu. Rekodi hiyo inashikiliwa na Mhangari Laszlo Kiss aliyefunga ndani ya dakika saba na sekunde 42 dhidi ya El Salvador katika Kombe la Dunia 1982.
WACHEZAJI WADOGO, WAKUBWA
Kwa wachezaji wadogo na wakubwa kufunga hat-trick
Edson Arantes do Nascimento maarufu Pele ndiye mchezaji mdogo zaidi kufunga katika fainali za Kombe la Dunia. Nyota huyo alifanya hivyo katika ushindi wa Brazil dhidi ya Ufaransa kwenye nusu fainali ya mwaka 1958 akiwa na miaka 17 na siku 244. Pia ndiye mchezaji pekee aliyefunga hat-trick akiwa chini ya miaka 18. Mchezaji mwingine mdogo kufanya hivyo ni Mjerumani Edmund Conen aliyefunga mabao matatu dhidi ya Ubelgiji 1934 akiwa na miaka 19 na siku 198.
Kwa upande mwingine, Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia, ambapo nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid alikuwa na miaka 33 na siku 130 alipofunga mabao yote matatu ya Ureno katika sare ya 3-3 dhidi ya Hispania 2018.
Bao lake la tatu lilikuwa mpira wa adhabu alioupiga kwa ustadi mkubwa dakika mbili kabla ya mwisho wa mchezo. Hat-trick hiyo ilikuwa ya 51 kwake katika ngazi ya klabu na timu ya taifa, na pia ilikuwa hat-trick ya 51 katika historia ya Kombe la Dunia.
HAT-TRICK ZAO HAZIKUSAIDIA
Katika historia ya mashindano hayo kuna wachezaji watatu pekee waliowahi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia, lakini wakaondoka wakiwa wamefungwa ambao ni Ernst Wilimowski dhidi ya Brazil 1938, ambapo Poland ilifungwa mabao 6-5. Wilimowski hasa anastahili kuhurumiwa, kwani alifunga mabao manne yote ya Poland katika kipigo hicho cha 6-5 dhidi ya Brazil. Mwingine ni Josef Hugi dhidi ya Austria 1954 aliyeshuhudia Uswisi ikifungwa 7-5 na Igor Belanov dhidi ya Ubelgiji 1986 aliyeondoka uwanjani akiishuhudia Jamhuri ya Kisovieti ya Urusi ikifungwa 4-3 baada ya muda wa nyongeza.
Wengine wanaweza kusema kuwa Kylian Mbappé naye aliingia kwenye orodha hiyo baada ya kufunga hat-trick katika fainali ya 2022 dhidi ya Argentina, ingawa Ufaransa ilipoteza kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya 3-3. Mchezaji mwingine pekee aliyefunga hat-trick bila kushinda ni Cristiano Ronaldo dhidi ya Hispania 2018 ambapo mchezo uliisha kwa sare ya 3-3.
HAT-TRICK NYINGI
Historia ya mashindano hayo inaonyesha kwamba kuna wakati kulikuwa na hat-trick nyingi zaidi katika Kombe la Dunia, ambapo Just Fontaine ni mmoja wa wachezaji watatu waliowahi kufunga katika mechi mbili tofauti za msimu mmoja wa mashindano hayo. Wengine ni Sandor Kocsis 1954 na Gerd Muller 1970. Muller alifunga hat-trick mbili mfululizo dhidi ya Bulgaria na Peru katika Kombe la Dunia nchini Mexico 1970.
Mchezaji mwingine aliyefunga hat-trick katika matoleo mawili tofauti ya Kombe la Dunia ni Gabriel Batistuta aliyetupia dhidi ya Ugiriki 1994 na Jamaica 1998.
Cha kushangaza, hat-trick zake zote mbili zilifungwa Juni 21, na zote zilikuwa dhidi ya mataifa yaliyoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, na bao la mwisho la kukamilisha hat-trick lilitokana na penalti.
MWAKA WA HAT-TRICK
Inaonekana ilikuwa rahisi zaidi kufunga hat-trick katika mashindano ya zamani ya Kombe la Dunia, na sababu inaweza kuwa sheria zilizowapa faida washambuliaji pamoja na tofauti kubwa ya viwango kati ya mataifa. Kati ya hat-trick 54 zote za Kombe la Dunia, 26 zilifungwa katika mashindano manane ya mwanzo, huku 28 zilizobaki zikisambaa katika michuano 14 iliyofuata licha ya kuwa na mechi nyingi zaidi.
Karibu asilimia 15 ya hat-trick zote zilifungwa katika Kombe la Dunia 1958 pekee, ambapo kulikuwa na hat-trick nane ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea katika toleo moja. Kombe la Dunia pekee ambalo halikushuhudia hata hat-trick moja ni lile la mwaka 2006 nchini Ujerumani.
JUMAPILI YA HAT-TRICK
Jumapili ndiyo siku iliyoshuhudia hat-trick nyingi zaidi katika Kombe la Dunia zikiwa ni 23 ambayo ni zaidi ya mara mbili ya siku inayofuata ambayo ni Jumamosi yenye 11. Kila siku ya wiki imeshuhudia hat-trick, lakini ni moja tu iliyowahi kufungwa Jumatatu. Hat-trick hiyo ilifungwa na Pauleta dhidi ya Poland 2002.
HAT -TRICK FAINALI
Geoff Hurst alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick katika fainali ya Kombe la Dunia aliyoifungia England dhidi ya Ujerumani Magharibi 1966 katika Uwanja wa Wembley na kuisaidia England kushinda 4-2 ikitwaa taji pekee la dunia.
Kylian Mbappe mchezaji mwingine pekee kufanya hivyo baada ya kufunga mabao matatu katika fainali 2022. Hata hivyo, haikutosha kwani Argentina ilibeba ubingwa kwa penalti baada ya sare ya 3-3.