Rekodi tamu za CP3 akisepa NBA
Muktasari:
Ligi hiyo imeshuhudia mwanzoni tu mwa mwaka huu supastaa Chris Paul maarufu CP3 akisepa baada ya kuitumikia kwa takriban miaka 21.
KIZAZI cha mastaa wa mwanzoni mwa miaka 2000 katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), ndiyo kinaondoka taratibu katika mashindano hayo ambayo yamekuwa yakichagizwa na ushawishi wa nyota kutoka mataifa mbalimbali.
Ligi hiyo imeshuhudia mwanzoni tu mwa mwaka huu supastaa Chris Paul maarufu CP3 akisepa baada ya kuitumikia kwa takriban miaka 21.
CP3 ni mchanganyiko wa herufi za majina yake na namba ya jezi yake. Pia anajulikana sana kama “The Point God”, jina linaloonyesha ubora wake wa hali ya juu wa kupanga mashambulizi, kupiga pasi na ufanisi wake kama mmoja wa ‘point guard’ bora zaidi katika historia ya NBA.
CP3, awali lilitolewa na babu yake na kudumu kupitia herufi zake za majina na nambari 3 ambayo ameivaa katika taaluma yake yote. Kwa upande mwingine, The Point God linatumiwa na mashabiki na wachambuzi kuashiria kiwango chake cha juu cha udhibiti wa uwanja kama ‘mwanajeshi’ mchezoni.
Mchezaji huyo aliyewahi kuchaguliwa mara 12 kwenye All-Star anaondoka kwenye mchezo huo akiwa nafasi ya pili muda wote kwa asisti na kupora mipira (steals). Katika chapisho kwenye Instagram, Paul aliandika: “Hiki ndicho! Baada ya zaidi ya miaka 21 naachana na mpira wa kikapu. Napoandika haya, ni vigumu kujua nahisi nini hasa, lakini mara moja watu wengi wangeshangaa. Sina jibu lolote haha! Lakini zaidi ya yote nimejawa na furaha na shukrani kubwa! Ingawa sura hii ya kuwa ‘mchezaji wa NBA’ imefika mwisho, mchezo wa kikapu utaendelea kuwa sehemu ya DNA ya maisha yangu milele.”
NAMBA ZAKE
Mshindi huyo wa medali mbili za dhahabu za Olimpiki amechaguliwa mara nne kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya All-NBA, na anashika nafasi ya pili katika historia ya NBA kwa asisti akiwa nazo 12,552 na uporaji wa mipira (steals 2,728). Vilevile alikuwa mchezaji wa kwanza kufikisha angalau pointi 20,000 huku akiwa na asisti 10,000 au zaidi.
Paul anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji waliopata mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Los Angeles Clippers akiiongoza kwenye misimu sita ya ushindi kuanzia 2011 hadi 2017, ambapo ilibeba mataji flani ya kawaida na makubwa ikiwemo mawili ya kwanza ya Pacific Division na ushindi mfululizo wa ‘playoff’ mara tatu.
Msimu huu alikuwa na wastani wa pointi 2.9 na asisti 3.3, akicheza dakika 14.2 kwa mchezo ikiwa ni viwango vya chini kabisa katika taaluma yake na hakushiriki kabisa katika michezo mitano mfululizo katikati ya Novemba, mwaka jana.
Safari ya ajabu ya mpira wa kikapu ya Paul ilijengwa katika juhudi zisizochoka. Point guard huyo mwenye ushupavu aligeuka kuwa gwiji wa NBA kupitia mchanganyiko wa ubora ndani na nje ya uwanja, akili na dhamira.
Alipata jina la utani lenye hadhi ya juu (Point God), kiasi kwamba lilionekana kama alibuni nafasi aliyocheza. Sivyo ilivyo. Paul aliifafanua nafasi hiyo vizuri zaidi kuliko wengi katika historia ya NBA na bila shaka katika kizazi chake.
Ndiyo maana aliitwa “Point God” akiwa ni point guard aliyedumu karibu miaka 21 katika ligi inayotawaliwa na wachezaji warefu, licha ya kuwa na urefu wa futi 6, mchezaji ambaye karibu kila wakati alijua nini cha kufanya akiwa na mpira mikononi na wakati gani wa kufanya majaabu uwanjani.
Akili na ujuzi aliokuwa nao vilikuwa mchanganyiko usiozuilika kwa CP3. Pia vilimwezesha kushinda changamoto ya urefu wakati ambapo wachezaji warefu na wenye nguvu zaidi walipoanza kutawala nafasi iliyokuwa ya wachezaji wafupi. Paul alikwenda kinyume na mwenendo huo na akaonyesha mara kwa mara kwa nini alikuwa kipaji cha kizazi cha aina yake.
KWANINI KASEPA?
Inaelezwa kwamba Paul ameamua kuondoka katika ligi hiyo akiwaacha wakongwe wenzake kina LeBron James na James Harden (Madevu), baada ya kuona kwamba mambo flani anapishana nayo uwanjani ikiwamo majeraha ya mara kwa mara, kukosa namba kikosini na pia ukaribu wake kwa wanawe ambao nyakati zao wakiwa likizo yeye anakuwa mzigoni.
Anasema msimu uliopita katika kipindi cha kiangazi alichukia kukosa matukio na fursa za kuwa karibu na watoto wake wakati wa likizo na hii imekuwa kawaida katika miaka ya hivi karibuni, na sasa baada ya kuamua kujiweka kando na kikapu uwanjani anaweza kujitolea zaidi kwa ajili ya familia na mambo mengine anayopenda kufanya.
Katika dirisha lililopita la usajili lililofungwa mwanzoni mwa Februari, mwaka huu, nyota huyo alihamishwa dakika za mwisho mwisho kwenda Toronto Raptors, timu pekee NBA inayotoka nchini Canada, lakini ilikuwa hatua ambayo haikuhitaji aripoti katika timu hiyo, kwani angeendelea kuishi Marekani na angeenda Toronto tu siku za mechi.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Raptors wameafiki kumuachia Paul na walijua asingecheza Toronto, na hilo lilizua maswali iwapo gwiji huyo wa Chuo Kikuu cha Wake Forest angejaribu kumaliza msimu akiwa na timu nyingine akitafuta kitu ambacho hakuwahi kupata ambacho ni ubingwa wa NBA.
ANAKUMBUKWAJE?
Kufunga pointi? Paul alikuwa bora katika kumiliki sanaa ya uchezaji iliyoanza kupotea tangu walipoondoka kina Michael Jordan, Allen Iverson na miaka ya karibuni Kobe Bryant , ambapo aliugeuza mchezo kuwa rahisi na kufunga au kutoa asisti kwake kilikuwa kitu chepesi.
Mwamba huyo alikuwa bora katika mitupo ya umbali wa kati (mid-range) na ya futi 18 ambayo ilichochea mikimbio ya wachezaji wenzake kupambania pointi kwa timu yake na kuwaumiza wapinzani. Pia alihusika kurusha karibu asilimia 90 ya mipira ya adhabu ambayo ni nadra kwamba haikuzaa matunda.
Udhibiti wa mpira (handles)? Alikuwa nao kwa kiwango cha juu, akijitoa kwenye presha na kujitengenezea nafasi nzuri mara kwa mara. Urefu wake wa kawaida ulikuwa faida katika hili; wachezaji wachache waliweza kuinama na kumnyang’anya mpira, lakini iliwalazimu kufanya kazi ya ziada.
Kupiga pasi? Alikuwa mmoja wa wachezaji wachache wa kulinganishwa nao. Mtazamo wake uwanjani ulikuwa wa kipekee na alielewa tabia za wachezaji wenzake. Alikuwa na kipaji cha kutoa pasi sahihi kwa mchezaji sahihi ili kuongeza uwezekano wa kufunga.
Ulinzi? Hapa ndipo aliposimama kwa kushangaza. Hofu ya wachezaji wafupi kuteswa kiulinzi haikumwandama. Alijua kuziba njia za pasi na kuiba mipira kwa ujanja wa hali ya juu kutoka kwa washambuliaji wa timu pinzani.
Uongozi? Huenda huo ulikuwa mchango wake mkubwa zaidi. Paul mara chache alidanganywa na hali ya mchezo. Wachezaji wenzake walifuata kile alichokuwa akiwaambia na ndicho kilichowasaidia kupata ushindi mchezoni. Hii ndiyo sababu alichaguliwa mara 11 kwenye All-NBA na mara tisa kwenye All-Defensive, akaongoza ligi kwa asisti mara tano (akiwa wa pili muda wote kwa jumla) na kupora mipra mara sita (pia wa pili muda wote kwa ujumla).
Paul alikuwa injini katika miaka sita aliyokuwa Los Angeles Clippers akitoa burudani. Pia aliifikisha fainali ya NBA kwa mara yake ya kwanza na pekee akiwa Phoenix Suns. Aliendelea kung’ara hata akiwa kwenye miaka ya mwishoni mwa 30.
Hata hivyo, Paul anaungana na kundi la mastaa wakubwa walioondoka NBA bila ubingwa kama John Stockton, Karl Malone, Charles Barkley na Patrick Ewing.
Kama alivyosema katika chapisho lake la kustaafu, “kucheza mpira wa kikapu kama kazi imekuwa baraka isiyoelezeka, iliyokuja pia na majukumu mengi. Nilikubali yote mazuri na mabaya. Inafurahisha kujua niliuheshimu mchezo tangu siku baba yangu aliponitambulisha. Mchezo ulikuwa daima sababu ya mimi kujitokeza. Na viongozi wa kweli na wapiganaji wanajua kwamba kujitokeza ni nusu ya vita.”
MSIKIE BOSI NBA
Kamishna wa NBA, Adam Silver amemsifia Paul kwa nidhamu ya kazi na nafasi yake ya zamani kama rais wa Shirikisho la Wachezaji wa Kikapu, akisema aliwarahisishia katika mazungumzo ya mikataba na dili mbalimbali za wachezaji.
“Baada ya misimu 21 ya ajabu, Chris Paul anastaafu kama mmoja wa point guard bora zaidi katika historia ya NBA na mlezi wa kweli wa mchezo wetu,” Silver alisema katika taarifa na kuongeza:
“Tangu alipoingia katika ligi, Chris alijitofautisha kwa uwezo wake wa kupanga mashambulizi, ushindani wa kiwango cha juu na maadili ya kazi. Pia alitumia muda na nguvu nyingi katika nafasi yake kama rais wa shirikisho la wachezaji akitoa mawazo yenye busara na misingi imara ili kuimarisha mchezo na biashara.
“Uongozi wake kwa niaba ya wachezaji ulikuwa muhimu katika mazungumzo ya mikataba ya pamoja, kusaidia ligi kupita kipindi cha majanga, kushughulikia masuala muhimu ya kijamii na mengine mengi. Kwa niaba ya NBA, nampongeza Chris kwa taaluma ya kipekee na kumshukuru kwa urafiki, ushirikiano na mchango wake wa kudumu katika mchezo wetu.”