Mayweather, Pacman mtasubiri sana!
Muktasari:
- Licha ya changamoto hizo, Marthur anaamini marudiano ya Mayweather na Pacquiao bado yatafanyika baadaye, lakini kwanza ni lazima migogoro yote ya kisheria itatuliwe ili kuweka msingi mzuri wa kuandaa pambano hilo upya.
WASHINGTON, MAREKANI: MCHAKATO wa kurejea ulingoni kwa Floyd Mayweather Jr unaendelea kukumbwa na changamoto, huku mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya promosheni ya Manny Pacquiao, Jas Marthur, akieleza sababu zilizofanya marudiano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Septemba kuahirishwa.
Akizungumza na Ring Magazine, Marthur amesema: “Pambano la Septemba limeahirishwa rasmi. Halitafanyika mwezi Septemba kutokana na kesi mbalimbali na matatizo ya kisheria yanayoendelea kwa sasa. Takribani siku 10 zilizopita, CSI waliweka mambo hadharani. Haya ni masuala ambayo yalikuwa yakijaribiwa kutatuliwa kimyakimya, lakini sasa mengi yamefahamika.”
Marthur ameongeza kuwa bado watu wengi hawaelewi jinsi hali hiyo ilivyotokea kwa sababu mikataba mbalimbali ilishafanyika na kukubaliana.
“Mapambano ya Floyd dhidi ya Mike Tyson, kurejea kwake kwenye ngumi za kulipwa, pambano dhidi ya Manny Pacquiao pamoja na pambano lililopangwa kufanyika Ugiriki yote yalifungamana kutokana na jinsi mikataba ilivyoandaliwa na jinsi makubaliano yalivyopangwa vibaya,” amesema.
Marthur pia amefafanua kuhusu fedha za awali ambazo Mayweather alidaiwa kupokea akisema hazikuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti binafsi ya Mayweather, bali zilitumwa kwa kampuni ya Frist Apex Ventures LLC ambayo ilikuwa imepewa mamlaka ya kusimamia haki za biashara za Mayweather.
Kwa mujibu maelezo yake, sehemu kubwa ya fedha hizo zilipaswa kumfikia Mayweather, lakini hapo ndipo matatizo yalipoanzia.
“Kulikuwa na migogoro mingine ya zamani isiyohusiana na pambano la Manny Pacquiao. Fedha zilikuwa zinaingia, lakini upande mmoja ulidai zilitumika kwa mambo fulani, huku Floyd akisema hakuwahi kuzipokea,” amesema Marthur.
Pia ameeleza kuwa awali kampuni ya CSI ilinunua haki za kuandaa pambano la maonyesho kati ya Mayweather na Mike Tyson na wakati huohuo, kampuni ya EverWonder ilikuwa ikijadiliana kuhusu pambano rasmi la Mayweather dhidi ya Pacquiao.
Tatizo lilitokea pale meneja wa biashara wa Mayweather alipowasilisha kwa CSI kuwa pambano la kurejea kwa Mayweather lingekuwa dhidi ya Pacquiao, wakati ukweli ni kwamba Pacquiao alikuwa bado hajasaini makubaliano na CSI.
Wakati huohuo, EverWonder ilikuwa tayari imesaini mkataba na Mayweather na hata kulipa fedha za awali.
Kutokana na hali hiyo, Marthur amesema: “Pambano lilelile liliuzwa mara mbili.”
Amefafanua kuwa ingawa maelezo ya wapinzani yalitofautiana kidogo kwenye mikataba, makubaliano yote mawili yalihusu pambano la kurejea kwa Mayweather kwenye ngumi za kulipwa, jambo lililosababisha mgongano wa kisheria.
Kwa upande wa Pacquiao, Marthur amesema maandalizi yalikuwa yanakwenda vizuri kwa sababu uamuzi ulikuwa ukifanywa na watu wachache, tofauti na upande wa Mayweather ambao ulikuwa na migogoro mingi.
Licha ya changamoto hizo, Marthur anaamini marudiano ya Mayweather na Pacquiao bado yatafanyika baadaye, lakini kwanza ni lazima migogoro yote ya kisheria itatuliwe ili kuweka msingi mzuri wa kuandaa pambano hilo upya.