Reijnders: Jamani mimi sio De Bruyne
Muktasari:
- Reijnders, 27, alijiunga na Man City kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 46 milioni akitokea AC Milan na amekuwa na kiwango kizuri, akifunga mabao matatu na kuasisti mara sita katika mechi 27 alizocheza msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa Manchester City, Tijjani Reijnders amewaambia mashabiki wake kwamba yeye sio Kevin De Bruyne mpya.
Reijnders, 27, alijiunga na Man City kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 46 milioni akitokea AC Milan na amekuwa na kiwango kizuri, akifunga mabao matatu na kuasisti mara sita katika mechi 27 alizocheza msimu huu.
Kiwango chake kiungo huyo kimemfanya aanze kulinganishwa na gwiji wa Man City, De Bruyne, 34, ikiwa ndiyo kwanza anaanza maisha yake huko Etihad.
Licha ya staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi kudai kwamba hiyo ni heshima kubwa, amesema yeye bado hajafika kwenye ubora wa De Bruyne, ambaye kwa sasa anakipiga huko Napoli baada ya kuitumikia Man City kwa miaka 10 na kuachana naye mwishoni mwa msimu uliopita.
Reijnders amesema kwamba klabu ilimweleza mapema kabisa wakati anawasili kwenye timu hiyo kwamba hawamtazami kama mtu wa kuja kuziba pengo la staa huyo wa Kibelgiji. Reijnders anamudu vyema kwenye Namba 8 ukilinganisha na De Bruyne, aliyekuwa matata kwenye Namba 10.
Reijnders amesema: “Baada ya mechi yangu ya kwanza dhidi ya Wolves, wachambuzi walianza kunilinganisha na Kevin De Bruyne. Ni heshima kubwa, lakini wajibu wangu ni tofauti na viwango vyangu ni tofauti.
“Man City iliniambia mwanzoni kabisa, nicheze mimi kama mimi, na nilijisema mimi sio De Bruyne mpya. Mimi ni kiungo ninayeweza kucheza eneo kubwa, lakini najiona mwenyewe kama Namba 8.”