Msikieni Guardiola anayesemwa anasepa
Muktasari:
- Kumekuwa na uvumi ni kwamba Guardiola amepanga kuachana na miamba hiyo ya Etihad wakati wa dirisha la majira ya kiangazi la mwakani.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Pep Guardiola amesema anafurahia kuwa kocha wa Manchester City licha ya kuwapo na uvumi unaozagaa kwamba ataachana na miamba hiyo ya Etihad mwishoni mwa msimu.
Kumekuwa na uvumi ni kwamba Guardiola amepanga kuachana na miamba hiyo ya Etihad wakati wa dirisha la majira ya kiangazi la mwakani.
Tangu wiki iliyopita kumekuwa la ripoti kwamba Man City imeshaanza kumtolea macho kocha wa Chelsea, Enzo Maresca wakimwona kuwa mtu sahihi wa kwenda kurithi mikoba ya Mhispaniola huyo huko Etihad.
Mkataba wa Guardiola kwenye kikosi cha Man City utafika tamati majira ya kiangazi 2027, akiwa aliusaini Novemba mwaka jana. Man City ilimwajiri Guardiola kwa mara ya kwanza 2016, jambo linalomfanya Mhispaniola huyo mwenye umri wa miaka 54 kuwa kocha aliyedumu kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu England kwa waliopo kwa sasa atakuwa amekamilisha muongo mmoja wakati msimu huu utakapofika mwisho.
Alipoulizwa kama ataendelea kuwa kocha wa Man City msimu ujao, Guardiola alijibu: "Nipo hapa.
“Miaka mitatu au minne iliyopita kuna mtu aliniuliza hilo swali. Nitakapofika miaka 75 au 76, nitaondoka Man City."
Guardiola aliongeza: “Naelewa msingi wa hilo swali, kwa sababu nimebakiza miezi 18 kwenye mkataba wangu, lakini mimi nina furaha. Hili swali naulizwa kila msimu na mimi niko sawa tu. Kinachokwenda kutokea kitatokea na klabu nimejiandaa kwa kila kitu. Klabu imejiandaa, lakini mjadala huo haupo mezani kwa sasa.”
Mkataba wa Maresca huko Chelsea utafika tamati majira ya kiangazi 2029 na kuna kipengele cha kumwongezea mwaka zaidi wa kuendelea kubaki Stamford Bridge.